Rais wa Kenya: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halifai, libadilishwe
Takwa la muda mrefu la viongozi wengi hususan kutoka Barani Afrika la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililoundwa tarehe 25 Octoba mwaka 1945 kufanyiwa marekebisho makubwa limeendelea kuchukua nafasi katika hotuba za viongozi wa ngazi za juu wanaohutubia katika mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la UN jijini New York ambapo Rais William Ruto wa Kenya amesema sababu zote za kulifanyia marekebisho baraza hilo zipo wazi.
Ruto amesisitiza katika hotuba yake kwa kusema: "iwapo uthibitisho wowote uliwahi kuhitajika kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halina utendaji kazi mzuri, halina demokrasia, sio jumuishi, halina uwakilishi na kwa hivyo halina uwezo wa kuleta maendeleo ya maana kwenye ulimwengu wetu kama ilivyo sasa, kutokujali kwa baadhi ya watendaji duniani kunathibitisha suala hilo".
Rais wa Kenya ametumia dakika 23 za hotuba yake kugusia masuala mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, hitaji la kuwa na ushirikiano, malengo ya maendeleo endelevu na migogoro inayoendelea katika maeneo mbalimabli duniani.
Ruto ametilia mkazo pia suala la mabadiliko katika taasisi za fedha ambapo ametaka yafanyike mageuzi katika taasisi za fedha za kimataifa, akibainisha kuwa, kwa mujibu wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kufikia mwezi uliopita wa Agosti, nchi 10 za kipato cha chini zilikuwa na dhiki ya madeni, na 52 ziko katika hatari kubwa na ya wastani ya kuangukia katika dhiki.../