Waislamu Kenya wapinga hatua ya Mahakama ya Juu kuruhusu mashoga kusajiliwa
-
Sheikh Abdullatif Essajee
Viongozi na wasomi wa dini ya Kiislamu wa Kenya wamelaani vikali uamuzi wa Mahakama ya Juu kuruhusu makundi ya mashoga na wasagaji kusajiliwa.
Wakihutubu katika Msikiti wa Jamia mjini Nairobi, mashekhe na wasomi wa Kiislamu wamesema uamuzi huo utawafanya Waislamu na Wakenya kupoteza imani na utendakazi wa mahakama hiyo.
Naibu Mwenyekiti wa Msikiti wa Jamia, Sheikh Abdullatif Essajee na msomi wa dini Sheikh Ahmadnur Mohamed waliongoza waumini kulaani uamuzi wa mahakama hiyo wakisema, unaenda kinyume na imani za dini na hata tamaduni za jamii mbalimbali nchini.
Sheikh Essajee amesema kuwa uamuzi huo unaenda kinyume na Katiba ya Kenya ambayo inapendekeza kifungo cha hadi miaka 14 kwa mashoga na wasagaji. Sheikh Essajee ameyasifu mataifa jirani ya Uganda na Tanzania kwa kusimama wima na kukataa kuruhusu makundi hayo licha ya mashinikizo ya baadhi ya nchi za kigeni.

“Inashangaza ni kwa msingi gani majaji hao walitoa uamuzi huo. Kama Waislamu tunapinga uamuzi huo”, amesema Sheikh Essanjee.
Miaka 10 iliyopita, Bodi ya Kushirikisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, ilikataa kusajili makundi ya mashoga kwa msingi kuwa yanaendeleza mapenzi ya jinsia moja.
Sheikh Abdullatif Essajee ameongeza kuwa: “Ni wazi kuwa kuna shinikizo za kuendeleza tabia za ushoga nchini kutoka kwa mataifa ya nje. Tunamuomba Rais William Ruto achukue msimamo wa kuharamisha hili jinsi walivyofanya wenzake Yoweri Museveni na Samia Suluhu.”
Sheikh Mohamed naye alisema, ushoga na usagaji hata umepingwa na dini za Uislamu na Ukristo kwa hivyo, uamuzi kuwa tabia hiyo imeruhusiwa hata umemshangaza yeye. Aliongeza kuwa tendo la ndoa limeruhisiwa kati ya watu ambao wameoana na lazima tu iwe ni mume na mke.