Sheikh Zakzaky: Zama za satwa ya madola ya Magharibi Afrika zimefikia ukingoni
Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa, matukio ya kisiasa ya Niger yanaonyesha kuwa, zama za satwa na ushawishi Ulaya na Marekani barani Afrika zimefikia tamati.
Sheikh Zakzaky amesema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na ripota wa Shirika la Habari la Iranpress huko Abuja, ambapo akizungumzia ufanisi wa serikali mpya ya Niger na maendeleo mapya ya kisiasa ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi, amesema, maendeleo haya ni ishara madhubuti ya watu kuchukua hatamu za uongozi.
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ameeleza kwamba, kuwepo kwa Ufaransa nchini Niger kumeifanya nchi hii kuwa maskini na sasa Niger ni nchi ya pili kwa umaskini zaidi duniani.
Kadhalika ameashiria kuwa Niger ina maliasili nyingi zikiwemo dhahabu na urani na kubainisha kwamba, Ufaransa inatumia rasilimali zote hizi kwa manufaa yake na Niger imeendelea kuwa maskini.

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema: Kitendo cha Ufaransa cha kuchimba migodi kimesababisha uchafuzi wa mazingira katika eneo la Afrika Magharibi na saratani imeongezeka na watu wanakufa kwa urahisi, lakini Ufaransa haisaidii hata kutoa dawa kwa wagonjwa.
Sheikh Ibrahim Zakzaky amesisitiza kuwa: Ulaya na Marekani lazima zielewe kwamba, zama za kutawala kwao Afrika na kuwa na satwa zimefikia tamati na hivi sasa Waafrika wanazidi kufanya harakati za kukabiliana na ubeberu na kusema kuwa rasilimali za nchi za Kiafrika ni mali ya wananchi.