Wadukuzi wa Algeria washambulia mitandao ya Wizara ya Vita ya Israel
Kundi moja la wadukuzi la Algeria limejipenyeza na kushambulia mitandao ya kuhifadhi taarifa za Wizara ya Vita ya utawala haramu wa Israel.
Kundi hilo linalojiita 'Anonymous Algeria' limesema limefanikiwa kuchota data zenye ukubwa wa gigabaiti 10 kutoka katika mitandao ya Wizara ya Ulinzi ya utawala wa Kizayuni.
Limesema limekusanya taarifa muhimu za maafisa na vikosi tofauti vya jeshi la Israel, na vile vile mipango ya jeshi hilo vamizi linalokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.
Kundi hilo limechapisha majina, anuani, na taarifa kuhusu wazazi wa wanajeshi wa Israel waliodukuliwa kwenye shambulizi hilo dhidi ya mitandao ya Wizara ya Ulinzi ya Israel.
Jumbe zilizochapishwa na kundi hilo la wadukuzi wa Algeria zimetangaza kuwaunga mkono wananchi wa Palestina ambao wanaendelea kufanyiwa kila aina ya ukatili na utawala haramu wa Israel.
Moja ya jumbe hizo umesema: Sisi taifa na jeshi la Algeria tunasimama pamoja na Palestina. Aidha limetengaza kuunga mkono ukombozi wa ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni.
Kwa mujibu shirika la data na takwimu la Cyber Express, makundi yapatayo 100 yanaendeleza mashambulizi na vita vya kidijitali wakati huu wa mgogoro wa Hamas na Israel, ambapo asilimia 70 yanaunga mkono Palestina.
Baadhi ya makundi mengine ya udukuzi yaliyotangaza kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina mkabala wa Israel ni pamoja na KillNet, Anonymous Sudan, na Mysterious Team Bangladesh.