HRW yataka kushinikizwa Ethiopiai ili wahanga wa vita vya Tigray wapate haki
(last modified Fri, 03 Nov 2023 08:04:02 GMT )
Nov 03, 2023 08:04 UTC
  • HRW yataka kushinikizwa Ethiopiai ili wahanga wa vita vya Tigray wapate haki

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeutaka Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kuishinikiza serikali ya Ethiopia ili kuhakikisha kwamba wahanga wa vita vya Tigray wanapata haki.

Shirika hilo la haki za binadamu linasema kuwa, vikosi vya Eritrea vilivyoungwa mkono na serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed, vilifanya mauaji, udhalilishaji wa kingono, utekajinyara watu, kuzuia kazi ya usambazaji wa misaada ya kibinadamu na kazi ya mashirika ya uangalizi ya Umoja wa Afrika, kufuatia kutiwa saini mkataba wa amani.

Mkataba wa amani, uliosimamiwa na Afrika Kusini na Umoja wa Afrika mnamo Novemba 2 mwaka jana, ulihitimisha mapigano ya Tigray ila kutokea wakati huo, kumeibuka machafuko katika sehemu nyingine za nchi hiyo hasa katika jimbo la Amhara.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, ripoti ya Tume ya Kimataifa ya Wataalamu wa Haki za Kibinadamu kuhusu Ethiopia kwa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa inazituhumu pande zote katika mzozo huo, kwa kutenda ukatili kaskazini mwa Ethiopia.

 

Ripoti hiyo inasema kuwa, pande hizo mbili zilishiriki uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, licha ya makubaliano ya amani yaliyotiwa saini, karibu mwaka mmoja uliopita.

Akiwasilisha ripoti hiyo, mwenyekiti wa tume hiyo, Mohamed Chande Othman, alionya kwamba kushindwa kwa makubaliano ya mwaka jana ya kumaliza uhasama, kumevunja matumaini kwamba mkataba huo "utafungua njia ya kumaliza moja ya migogoro mibaya zaidi ya karne ya 21, ambayo imevuruga jamii kote kaskazini mwa Ethiopia.

Tume hiyo ya haki za binadamu kuhusu Ethiopia imesema katika jimbo la Amhara ambako serikali ilitangaza hali ya dharura mwezi uliopita, imekuwa ikipokea ripoti za makundi ya watu hasa raia kukamatwa kiholela na angalau kulikuwa na shambulio moja la ndege zisizo na rubani au drone lililofanywa na serikali.