May 09, 2024 07:17 UTC
  • Kenya yatangaza mapumziko nchi nzima Ijumaa ili kuwaomboleza wahanga wa mafuriko

Rais William Ruto wa Kenya ametangaza kesho Ijumaa kuwa ni siku ya mapumziko ili kuwaomboleza watu 238 waliopoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyoiathiri nchi hiyo.

Rais Ruto jana alitangaza kuwa kesho Ijumaa itakuwa siku ya kupanda miti ili kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Kenya pamoja na maeneo mengine ya Afrika Mashariki yameathiriwa pakubwa na mafuriko. Watu zaidi ya 235,000 wamelazimika kuhama makazi yao na sasa makumi ya watu wanaishi makambini. 

Mafuriko Kenya 

Rais Ruto pia ametangaza kufunguliwa shule kote nchini ifikapo tarehe 13 mwezi huu wa Mei, baada ya kuchelewa kwa wiki mbili kutokana na mvua kubwa zilizosababisha mafuriko na mamia ya shule kufungwa.

Serikali ya Kenya imesema kuwa shule zaidi ya 1,000 zimeathiriwa na mvua kubwa na kuwa tayari imetenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa shule hizo. 

Serikali iko mbioni kuwaondoa kwa nguvu watu wanaoishi katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko na wale walio karibu na mito na mabwawa huku viwango vya maji katika mabwawa makubwa ya kuzalisha umeme nchini humo yakipanda na kufikia "viwango ambavyo havijawashi kushuhudiwa."

Tags