Polisi 200 wa Kenya kupelekwa Haiti Alkhamisi ijayo
Polisi 200 wa Kenya watapelekwa nchini Haiti kulinda usalama siku ya Alkhamisi ijayo. Ni baada ya vuta nikuvute ya muda mrefu mahakamani, ambapo Januarii mwaka huu Mahakama ya juu nchini Kenya ilitangazwa kuwa, mpango wa serikali wa kutuma polisi nchini Haiti kuongoza kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa ni kinyume na katiba.
Hatimaye sasa imeamuliwa kuwa, kikosi cha kwanza cha maafisa 200 wa polisi ya Kenya kinatazamiwa kusafiri hadi nchini Haiti Alhamisi ijayo.
Kikosi hicho ni sehemu ya maafisa 1,000 walioidhinishwa na Umoja wa Mataifa kwenda kudumisha amani katika taifa hilo ambalo halijashuhudia utulivu kwa muda mrefu.
Ghasia za magenge ziliikumba Haiti miaka mingi iliyopita, lakini zimeongezeka zaidi tangu kuuawa Rais Jovenel Moise mnamo 2021. Umoja wa Mataifa unakadiria mzozo huo ulisababisha vifo vya takriban watu 5,000 mwaka jana na kupelekea wengine 300,000 kuhama makazi yao, huku kukiwa na uhaba wa chakula na huduma za matibabu.
Baadhi ya raia wa Haiti wanaoishi nje ya nchi wameshutumu Kenya kwa kukubali kutuma polisi nchini mwao kudumisha amani na kupambana na magenge ya wahalifu walioteka nchi hiyo.

Raia hao wa Haiti wamemtuhumu Rais William Ruto wa Kenya kuwa ni ‘kibaraka’ wa Marekani na kuitaka Washington iondoke nchini Haiti ikilaumiwa kwamba inayapa silaha magenge hayo.
Mwishoni mwaka jana pia kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, alikosoa uamuzi wa nchi hiyo kuongoza kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Haiti ili kukabiliana na ghasia za magenge ya uhalifu, akiitaja hatua hiyo kuwa haifai.
"Kwanini Kenya?", Odinga alihoji kwa kejeli, na kusema: "Marekani yenyewe iliondoa majeshi yake huko Haiti na tatizo la nchi hiyo ni la kisiasa; hivyo hawahitaji bunduki zaidi kutuliza hali mambo."
"Sidhani kama ni hatua sahihi. Swali tunalopaswa kuuliza ni kwa nini Kenya? Ni kitu gani kinachoitofautisha Kenya na nchi 54 za Afrika?", alihoji Raila Odinga na kusema kuwa mpango wa kutuma polisi nchini Haiti sio kipaumbele cha Kenya.