Mahakama Kenya yailaumu polisi kwa kifo cha mwandishi habari wa Pakistan
Mahakama nchini Kenya jana ilitoa uamuzi ikisema kuwa kitendo cha polisi wa nchi hiyo cha kumpiga risasi mwandishi wa habari wa Pakistan mjini Nairobi mwaka 2022 kilikuwa kinyume cha sheria na kinyume na katiba.
Jaji Stella Mutuku pia amemkosoa Mwanasheria Mkuu na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma wa Kenya kwa kuzembea kuchunguza kifo cha Arshad Sharif baada ya polisi kulimiminia risasi gari lalke katika kituo cha upekuzi cha trafiki.
Familia ya Arshad imeituhumu polisi ya Kenya kwa kumuua kwa makusudi ndugu yao. Mwandishi huyo wa habari Mpakistani aliyekuwa na umri wa miaka 50 alitoroka Pakistan mapema mwaka 2021 akikwepa kutiwa nguvuni kwa madai ya kuzidhalilisha taasisi za serikali ya nchi hiyo.
Mwezi Disemba 2022 kundi moja la wachunguzi kutoka Pakistan lilihitimisha ripoti yake kwamba kifo cha Sharif kilikuwa ni mauaji yaliyopangwa. Ripoti ya kundi hilo ilieleza kuwa risasi iliyomjeruhi vibaya Sharif ilifyatuliwa kutoka ndani ya gari au katika eneo la karibu.

Mamlaka husika za Kenya zinaendelea kuchunguza mauaji hayo, ambapo hadi sasa hakuna afisa yeyote wa polisi aliyehusika katika ufyatuaji risasi ambaye amekamatwa au kufunguliwa mashtaka.
Katika uamuzi wake wa Jumatatu, mahakama nchini Kenya imeziagiza mamlaka husika kukamilisha uchunguzi wao kuhusu maafisa hao wa polisi. Pia imeiamuru serikali kuilipa fidia familia ya Sharif kiasi cha hadi shilingi milioni 10 za Kenya, sawa na dola 78,000.
Dudley Ochiel, Wakili wa mjane wa Sharif, Javeria Siddique, alisema jana kuwa uamuzi uliotolewa na mahakama ni "ushindi mkubwa kwa familia na marafiki wa Arshad Sharif huko Kenya, Pakistan na duniani kote".