Mashinikizo ya vijana yamlazimisha Ruto alivunje Baraza la Mawaziri
Rais William Ruto wa Kenya ametangaza kulivunja Baraza la Mawaziri kutokana na mashinikizo na maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen-Z. Kwa mujibu wa sheria za Kenya, Rais hana mamlaka ya kumfuta kazi Naibu wake.
Akihutubia taifa kutoka Ikulu ya Nairobi leo Alkhamisi, Ruto ametangaza kulivunja baraza lote la mawaziri, huku Waziri Kiongozi, Musalia Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo akiponea kuangukiwa na shoka hilo. Aidha Rais wa Kenya amempiga kalamu nyekundu Mwanasheria Mkuu, Justin Muturi.
Ameeleza kuwa, Ofisi ya Naibu Rais, Rigathi Gachagua haitaathiriwa na uamuzi aliotangaza leo. Ruto amesema, baada ya kufanya mashauriano ya kina, kusikiza miito ya wananchi, na kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa na sheria, ameamua kulivunja baraza lote la mawaziri, isipokuwa Ofisi ya Waziri Kiongozi, Musalia Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.
Dakta Ruto amesema: “Leo hii, kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na Ibara ya 152(1) na 152(5) B ya Katiba na Kifungu cha 12 cha Sheria ya Mwanasheria Mkuu, nimeamua kuwafuta kazi mara moja mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Kenya.”
Dakta Ruto amesema shughuli za serikali zitaendelea bila kutatizwa, kwa kusimamiwa na Makatibu wa Wizara, huku akiapa kuwa serikali yake imeazimia kupambana kwa nguvu zote na jinamizi la ufisadi. Amesema baraza jipya la mawaziri litatangazwa baada ya kufanya mashauriano ya kina na wadau na wataalamu wa sekta husika.

Tangazo hilo ni katika mfululizo wa hatua alizochukua Dakta Ruto karibuni kujaribu kutuliza joto na ghadhabu za vijana ambao wamekuwa wakiandamana kwa wiki kadhaa sasa wakilalamikia uongozi mbaya wa serikali ya Kenya Kwanza. Wiki iliyopita, Ruto alipendekeza kupunguzwa kwa matumizi ya serikali na kukopa pesa nyingi zaidi ili kujaza nakisi ya bajeti ya takriban dola bilioni 2.7.
Aidha juzi Jumanne, Rais Ruto alisaini muswada wa marekebisho ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wa 2024 kuwa sheria, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta (KICC) jijini Nairobi mbele ya viongozi wa upinzani Raila Odinga (ODM), Kalonzo Musyoka (Wiper), Naibu Rais Rigathi Gachagua na viongozi wa Bunge la Kitaifa na Seneti. Hatua hiyo sasa inapisha rasmi uteuzi wa jopo la uteuzi litakaloajiri makamishna wapya wa tume ya uchaguzi.
Vijana wa Gen-Z walianza kufanya maandamano mwezi uliopita kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 ambao ungechangia kuongezwa kwa viwango vya ushuru; lakini yabadilika na kuwa maandamano ya kukosoa utawala mbaya wa Rais Ruto.