Raia wote wa kigeni watakiwa kuondoka Khartoum, Sudan
(last modified Sat, 13 Jul 2024 07:05:32 GMT )
Jul 13, 2024 07:05 UTC
  • Raia wote wa kigeni watakiwa kuondoka Khartoum, Sudan

Vyombo vya usalama nchini Sudan vimewataka raia wote wa kigeni kutoka katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum pamoja na viunga vyake.

Taarifa ya vyombo vya usalama imewapatia raia wa kigeni muhula wa wiki mbili wawe wameshaondoka Khartoum.

Maagizo hayo yanakuja huku kukiwa na mapigano ambayo bado yanaendelea kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka, na sanjari na kuanza tena juhudi za kikanda na kimataifa za kutatua mzozo huo.

Mkurugenzi wa Idara ya Wageni na Udhibiti wa Uhamiaji katika Jimbo la Khartoum, Kanali Nizar Khalil, amewapa wageni wote muhuula wa "siku 15 kuondoka Khartoum ili kulinda maisha yao wakati wa vita."

Amedokeza kuwa uamuzi huo umechukuliwa kwa kuzingatia maagizo ya Kamati ya Kuratibu Usalama ya Jimbo la Khartoum.

Makamanda hasimu wa kijeshi ambao wameitumbukiza Sudan katika vita vya wenyewe kwa wenyewe

 

Polisi walihalalisha amri hizi kwamba ni kulinda usalama wa wageni ambao hawajaondoka Khartoum, licha ya kuwa imekuwa ikishuhudia mapigano makali tangu Aprili 2023.

Wakati huo huo mkuu wa Baraza la Utawala wa Kijeshi wa Sudan, Abdel Fattah Al-Burhan, amekanusha kuwepo kwa mazungumzo yoyote ya kusitisha mapigano.

Al-Burhan alisisitiza kuwa usitishaji vita wowote unategemea kuondoka kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka kutoka miji ya El Geneina, Zalingei, El Fasher, El Daein na Jimbo la Al-Jazira, na Jimbo la Sennar.

Sudan ilitumbulia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Aprili 15, kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na Abdel Fattah al-Barhan na Vikosi vya Msaada wa Dharura (RSF) chini ya amri ya Mohammed Hamdan Dagalo.