HAMAS: Hatutajifunga kukabidhi silaha mpaka yatakapofanyika mazungumzo zaidi
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesisitiza kuwa haitajifunga moja kwa moja kukabidhi silaha na inatumai usitishaji vita na utawala wa kizayuni wa Israel utadumu kwa muda wa miaka mitatu hadi mitano ili kuijenga upya Ghaza.
Msimamo huo umetangazwa na mjumbe mwandamizi wa ofisi ya kisiasa ya harakati hiyo ya ukombozi wa Palestina Muhammad Nazzal katika mahojiano na shirika la habari la Reuters yaliyofanyika mjini Doha, Qatar.
Alipoulizwa kama Hamas itakabidhi silaha zake, Nazzal alisema: "Siwezi kujibu ndiyo au hapana. Kusema kweli, inategemea na aina ya mpango huo. Mpango wa kukabidhi silaha unaouzungumzia unamaanisha nini? Silaha hizo zitakabidhiwa kwa nani?"
Wanadiplomasia wa Kiarabu hapo awali walivieleza vyombo vya habari kwamba wapatanishi walikuwa kwenye majadiliano na Hamas kuhusu kukabidhi silaha zake kwa walinda amani wa nchi za Kiarabu au kuzifunga silaha zake za masafa marefu kama vile makombora badala ya kuziharibu.
Mpango wa amani wa vipengele 20 uliopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump unatoa wito kwa Hamas wa kubali bila kuwa na nguvu za kijeshi. Pia unatoa wito wa kuondoka kikamilifu lakini hatua kwa hatu jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza. Hata hivyo, mpango huo hautoi ratiba maalumu ya utekelezaji wa hatua zote hizo mbili.
Katika mahojiano hayo, Nazzal pia amesema Hamas watakuwa na "jibu la wazi" na la uhakika watakapofika kwenye meza ya mazungumzo kwa ajili ya awamu ya pili ya makubaliano hayo, na kwamba makundi mengine ya Palestina yatahitaji kushauriwa juu ya suala hilo.../