Sep 17, 2024 03:04 UTC
  • Wachimba dhahabu Kenya wapoteza maisha baada ya mgodi kuporomoka

Watu wasiopungua tisa wamepoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati mgodi usio rasmi wa dhahabu ulipoporomoka na kuwaangukia wachimba dhahabu hao huko kaskazini mwa Kenya karibu na mpaka wa Ethiopia.

Mamlaka husika ziliufunga mgodi huo wa dhahabu wa kujikimu wa Hillo karibu na mpaka wa Ethiopia mwezi Machi mwaka huu baada ya watu kadhaa kuuawa katika mapigano kati ya jamii za eneo hilo wakigombania ardhi ya uchimbaji lakini wachimba migodi walikaidi amri na kuendelea kuchimba madini katika mgodi huo. 

David Saruni Naibu Kamishna wa kaunti ya Marsabit amesema kuwa Jumatatu jioni watu wasiopungua 1000 waliwazidi nguvu askari usalama na kuvamia eneo hilo.

Naibu Kamishna wa kaunti ya Marsabit ameeleza kuwa, wavamizi hao walichimba eneo lililotelekezwa ambalo liliporomoka na kuwaangukia baadhi yao miongoni mwao.  

Naye Alio Guyo mzee wa kijiji amesema kuwa miili tisa imeondolewa katika vifusi hadi sasa ambayo imetajwa kuwa ni ya raia watano wa Kenya na wanne kutoka Ethiopia. 

Polisi katika kaunti ya Siaya imeeleza kuwa kuporomoka kwa migodi na maeneo ya uchimbaji  madini kumekuwa kukijiri mara kwa mara huko Kenya. Mapema mwezi huu, takriban watu saba walipoteza maisha baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka katika kaunti ya Siaya magharibi mwa Kenya.

Tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Lumba yapata umbali wa kilomita 400 kutoka mji mkuu wa Kenya, Nairobi. 

 

Tags