Kenya yaomba msaada wa China kujiunga na BRICS
(last modified Wed, 06 Nov 2024 13:32:53 GMT )
Nov 06, 2024 13:32 UTC
  • Kenya yaomba msaada wa China kujiunga na BRICS

Rais wa Kenya William Ruto ameomba China iunge mkono ombi la taifa hilo la Afrika Mashariki kujiunga na kundi hilo BRICS.

Taarifa zinasema ombi hilo limewasilishwa Jumatatu, wakati wa mazungumzo ya Ruto na Li Xi, katibu wa Tume Kuu ya Ukaguzi wa Nidhamu ya Chama tawala cha Kikomunisti cha China.

Katika kikao hicho Ruto aliipongeza Beijing kwa kufadhili "miradi ya kipaumbele," nchini Kenya.

Hatua hiyo ya Kenya imekuja wiki chache tu baada ya Russia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 16 wa wakuu wa nchi za BRICS mjini Kazan, ambao ulishirikisha wajumbe kutoka nchi kadhaa. Nchi za Magharibi hazikkupendezwa na mkutano huo ambao  ulidhihirisha kwamba, kinyume cha madai yao, Russia haijatengwa. Mkutano huo wa kila mwaka ulikuwa wa kwanza tangu upanuzi wa kundi hilo mapema mwaka huu, wakati Misri, Iran, Ethiopia, na Umoja wa Falme za Kiarabu zilipojiunga rasmi na Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini.

Mkutano wa BRICS huko Kazan nchini Russia

Kulingana na makadirio ya taasisi za fedha za kimataifa, nchi wanachama wa BRICS za sasa zinachukua karibu 46% ya watu duniani na zaidi ya 36% ya Pato la Taifa la kimataifa.

Wachambuzi wamekuwa wakiitaka serikali ya Kenya kujiunga na jumuiya hiyo ya kiuchumi baada ya Ethiopia na Misri kuwa wanachama, huku nchi nyingine kadhaa za Afrika, zikiwemo Algeria na Nigeria, zikionyesha zikiwa tayari zimeomba kujiunga na jumuiya hiyo.

Licha ya kuwa mshirika mkuu wa Marekani, Kenya imejaribu kuimarisha uhusiano na China na Russia, ambazo kuongezeka kwa uwepo wake barani Afrika kumezua wasiwasi katika nchi za Magharibi.