Mtaalamu: Kwa Afrika hakuna tofauti baina ya Trump na Harris
Huku Donald Trump akiwa amejitangaza kuwa mshindi katika uchaguzi wa Marekani, wataalamu wa mambo wanasema hakuna tofauti kwa Afrika kuhusu ni nani anayechukua hatamu za uongozi kati ya mgombea wa Wademokrat au Warepublican.
Moussa Ibrahim, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Turathi za Kiafrika, Johannesburg ameiambia RT kwamba iwe ile sera ya Trump ya 'Amerika Kwanza' au ujanja wa kidiplomasia wa Harris, mataifa ya Afrika lazima yatambue kwamba atakayekuwa rais wa Marekani ataleta tu mabadiliko ya kimbinu ndani ya mfumo ambao kwa muda mrefu imekuwa ikidhoofisha uhuru na kujitawala kwa Afrika.
Anasema Trump na Harris wote wanawakilisha sura mbili za sarafu moja. Mtazamo wa Trump ni butu na wa moja kwa moja. Anaahidi Marekani kutoingilia sana masuala ya Afrika lakini wakati huo huo analenga kuvuruga uchumi wake kwa kutekeleza hatua za kuzuia uagizaji wa bidhaa za Afrika. Amedokeza juu ya kupandisha ushuru wa asilimia 10 ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, ambao bila shaka utaathiri vibaya wauzaji bidhaa za Afrika ambao wanategemea masoko ya Marekani. Mbinu hii inaashiria kurejea kwa utaifa wa kiuchumi.
Kinyume chake, mbinu ya Harris imejikita katika mtindo laini lakini wa ukoloni mamboleo. Kupitia sisitizo lake juu ya mipango ya kile kinachodaiwa kuwa ni haki za binadamu na uwekezaji katika nishati ya kijani, Harris anaonekana kuunga mkono ushirikiano na Afrika.
Hata hivyo, uwekezaji huu ni wa kimkakati, unaolenga kuilazimisha Afrika kushikamana na maslahi ya Marekani, huku ukiweka kando vipaumbele vya nchi za Kiafrika katika maendeleo.
Ibrahim ameongeza kuwa Marekani ya Trump inaiona Afrika kama kipaumbele cha mwisho katika mtazamo wake wa ulimwengu wa kujitenga. Trump anaitazama Afrika kama bara la kupuuzwa au kunyonywa inapofaa. Ikumbukwe kuwa wakati akiwa rais, Trump aliwahi kuzifananisha nchi za Afrika, Haiti, Ecuador na 'Shimo la Choo'.
Msomi huyo amebainisha kuwa viongozi wa Marekani watakuja na kuondoka, lakini ukombozi wa Afrika utatoka ndani ya bara hilo tu bila kutegemea ni nani anayetawala Marekani.