Je, mfumo mpya wa kikanda unaofuatiliwa na Iran una sifa gani?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i126742-je_mfumo_mpya_wa_kikanda_unaofuatiliwa_na_iran_una_sifa_gani
Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefafanua mfumo mpya wa kieneo unaofuatiliwa na Iran, katika makala iliyochapishwa kwenye tovuti ya Jukwaa la Mazungumzo la Tehran.
(last modified 2025-05-24T02:32:27+00:00 )
May 24, 2025 02:32 UTC
  • Je, mfumo mpya wa kikanda unaofuatiliwa na Iran una sifa gani?

Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefafanua mfumo mpya wa kieneo unaofuatiliwa na Iran, katika makala iliyochapishwa kwenye tovuti ya Jukwaa la Mazungumzo la Tehran.

Mfumo huo mpya unajumuisha vipengele kadhaa vya msingi. Kipengele cha kwanza ni kwamba mfumo huo unasisitiza msingi wa kuwa huru na kujitegemea kitaifa badala ya kutegemea madola yenye nguvu duniani. Jambo ambalo limekuwa likienea na kuongezeka katika eneo la Asia Magharibi katika miongo ya hivi karibuni ni ushawishi wa madola ya kigeni, hasa madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani, pamoja na uingiliaji wao katika masuala ya kikanda. Uingiliaji huo umeongezeka kiasi kwamba hata madola hayo yamejipa haki ya kuteua na kuwaweka madarakani watawala wa nchi za eneo. Kile kinachosisitizwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jambo ambalo pia limekuwa likidhihiri taratibu katika siasa za nchi nyingine za eneo hili, hususan Saudi Arabia katika miaka ya hivi karibuni, ni kuheshimiwa mamlaka za kitaifa za kila nchi na kutoyategemea madola ya kigeni.

Sifa ya pili ya mfumo huu mpya wa kieneo unaosisitizwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kwamba ushirikiano madhubuti unapasa kuchukua nafasi ya miungano dhaifu. Kimsingi, eneo la Asia Magharibi ni mojawapo ya maeneo ambayo ni nadra kuona ushirikiano wa aina hii ukidumishwa kati ya nchi za kanda. Suala hili limechochea uingiliaji wa madola ya nje ya kanda na pia kusababisha ghasia na migogoro isiyomalizika katika eneo, jambo ambalo limezisababishia nchi hizo hasara na maafa makubwa. Ushirikiano dhaifu kati ya nchi za kanda, na hata kati ya nchi hizo zenyewe na tawala za nje ya kanda, haujaziletea usalama na utulivu wowote. 

Eneo la Asia Magharibi

Kubadilishwa miungano dhaifu na ushirikiano madhubuti baina ya nchi husika kwa upande mmoja kunaweza kuleta utulivu na usalama zaidi katika eneo, na kwa upande wa pili, kupunguza gharama za kijeshi na kiusalama za mataifa ya eneo, na pia kunaweza kuzuia uporaji wa mali na utajiri wa eneo, unaofanywa na madola ya Magharibi hususan Marekani.

Sifa ya tatu ya mfumo mpya wa kieneo unaofuatiliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kwamba badala ya kuzingatia usalama pekee, maendeleo ya kiuchumi yanapaswa kupewa kipaumbele. Kimsingi, mtazamo wa kiusalama tu kuhusu siasa na madaraka, na vile vile uhusiano na nchi za eneo fulani, huzifanya nchi za eneo hilo kutofikia maendeleo na ustawi unaohitajika, na badala yake huingia kwenye mchezo usiokuwa na manufaa yoyote kwao, kwa maslahi ya madola ya kibeberu na kikoloni ya Magharibi. Hii ni katika hali ambayo mtazamo wenye mwelekeo wa maendeleo wa siasa na nguvu unaweza kuandaa mazingira ya kupatikana maendeleo na ustawi zaidi wa kitaifa. Mtazamo wa aina hii bila shaka utaimarisha mashirikiano kati ya nchi na kuchochea mahusiano yenye matokeo chanya kwa manufaa ya eneo zima.

Sifa ya nne ya mfumo mpya wa kieneo unaotakiwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kwamba unadhamini usalama wa pamoja badala ya mifumo iliyowekwa na wahusika wa kigeni. Mfumo uliowekwa na waporaji wa kigeni unashajiisha mgawanyiko kati ya mataifa ili kutoa mwanya wa kuweza kutawaliwa na kudhibitiwa kutoka nje. Mfumo huu unakinzana kikamilifu na wito wa kuwepo ushirikiano kati ya mataifa, maendeleo na ustawi. Hii ni katika hali ambayo usalama wa pamoja, kwa upande mmoja, unazingatiwa katika matazamo wa usalama wa nchi zote za eneo, na kwa upande mwingine, unaandaa uwanja wa nchi husika kuaminiana zaidi na hivyo kuziletea mafanikio na maendeleo makubwa ya nchi binafsi na eneo zima kwa ujumla.