Trump aitishia EU kwa ushuru wa forodha wa 50%
(last modified Sat, 24 May 2025 06:51:39 GMT )
May 24, 2025 06:51 UTC
  • Trump aitishia EU kwa ushuru wa forodha wa 50%

Rais wa Marekani Donald Trump amependekeza "ushuru wa moja kwa moja wa 50%" kwa nchi zote za Umoja wa Ulaya, akitaja nakisi ya biashara ya dola milioni 250 kila mwaka na umoja huo. Amependekeza kuwa kiwango hicho kipya cha ushuru kianze kutekelezwa Juni 1.

Katika ujumbe kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Truth Social jana Ijumaa, Trump alipendekeza kwamba EU iliundwa mwanzoni "kwa madhumuni ya kimsingi ya kuchukua fursa ya Marekani kwenye Biashara," na amesisitiza kuwa umoja huo "umekuwa mgumu sana kushirikiana nao."

Amedai kwamba, sera za kiuchumi za EU, kodi, kanuni na "mashtaka yasiyo ya haki na uadilifu dhidi ya kampuni za Marekani" yamesababisha nakisi ya biashara na EU ya "zaidi ya dola milioni 250 kwa mwaka," ambayo alielezea kuwa "haikubaliki kabisa."

"Majadiliano yetu nao hayaendi popote! Kwa hivyo, ninapendekeza ushuru wa moja kwa moja wa asilimia 50 kwa Umoja wa Ulaya, kuanzia Juni 1, 2025," Trump ameeleza akiongeza kuwa, hakutakuwa na ushuru kwa bidhaa "zilizozalishwa au kutengenezwa nchini Marekani."

Mnamo Aprili, Trump aliweka ushuru mkubwa wa 20% kwa bidhaa zote za EU na vile vile ushuru wa 25% kwa uagizaji wa magari na madini yote ya chuma. Hata hivyo, baadaye alisimamisha ushuru wa 20% kwa siku 90, akiweka tu ushuru wa msingi wa 10%.

Mwezi uliopita wa Aprili, Shirika la Biashara Duniani (WTO) lilitahadharisha kuwa ushuru uliotangazwa na Trump utarudisha nyuma biashara ya kimataifa mwaka huu na kupelekea kushuka kwa kasi ukuaji wa uchumi wa dunia.