Harvard yaushtaki utawala wa Trump kwa kupiga marufuku wanafunzi wa kigeni
(last modified Sat, 24 May 2025 07:05:11 GMT )
May 24, 2025 07:05 UTC
  • Harvard yaushtaki utawala wa Trump kwa kupiga marufuku wanafunzi wa kigeni

Chuo Kikuu cha Harvard kimeushtaki utawala wa Donald Trump kwa kuizuia taasisi hiyo mashuhuri ya elimu ya Marekani kusajili wanafunzi wa kigeni, kikiitaja hatua hiyo kuwa ni ulipizaji kisasi kinyume na katiba, kutokana na wanachuo hao kukaidi amri za kisiasa za Ikulu ya White House.

Chuo hicho kiliwasilisha kesi Ijumaa asubuhi kikitaka kutolewa zuio la muda katika jaribio la kuzuia Idara ya Usalama wa Ndani ya Marekani kuwapiga marufuku wanafunzi hao wa kigeni.

Kufuatia ombi hilo, Jaji wa Marekani, Allison Burroughs alitoa amri ya zuio la muda na kufungia utekelezaji wa sera hiyo kwa muda wa wiki mbili.

Kwa mujibu wa faili la kesi hiyo, wanafunzi wa kigeni wanaoendesha maabara, kufundisha kozi, kusaidia maprofesa na kushiriki katika michezo ya Harvard sasa wameachwa katika njiapanda, wasijue iwapo watahamishwa au wanakodolewa macho na hatari ya kupoteza kibali cha kusalia nchini.

Harvard inasema hatua ya serikali ya Marekani inakiuka Ibara ya Kwanza na itakuwa na "athari za haraka na mbaya kwa chuo hicho na zaidi ya watu 7,000 wenye viza.

Haya yanajiri mwezi mmoja baada ya chuo hicho kufungua mashtaka mengine dhidi ya serikali ya Marekani kikitaka kumzuia Trump asisimamishe mabilioni ya dola ya bajeti ya Serikali ya Federali kwa chuo hicho na kulinda uhuru wake.

Trump alitaka kukata bajeti ya serikali kwa vyuo vikuu kama Harvard, Columbia na vyuo vingine ambavyo anadai vimeshindwa kudhibiti suala la chuki dhidi ya Wayahudi kwenye vyuo hivyo. Wanafunzi na walimu wa vyuo hivyo wamekuwa wakifanya maandamano na migomo wakipinga mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza, Palestina.

Tangu aliposhika madaraka mapema mwaka huu, Trump alianzisha kampeni kubwa ya kunyamazisha sauti zote zinazopinga sera za utawala katili wa Israel na maandamano yanayofanywa na wanafunzi wa vyuo vikuu kupinga mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israe hususan katika Ukanda wa Gaza.