Seneta wa Marekani: Mpango wa nyuklia wa Iran haujaangamizwa
-
Chris Murphy
Chris Murphy, Seneta wa Marekani wa chama cha Democratic amesema, madai ya rais wa nchi hiyo Donald Trump kuhusu kuangamizwa mpango wa nyuklia wa Iran hayana ukweli.
Murphy ameeleza hayo mbele ya waandishi wa habari baada ya kikao cha faragha cha Baraza la Seneti kilichoijadili Iran na akafafanua kwa kusema: “inavyoonekana, sisi tumeweza kuurudisha nyuma kwa miezi michache tu mpango wa nyuklia wa Iran. Madai ya rais kwamba tumeuangamiza kikamilifu mpango huo, si sahihi”.
Seneta huyo wa chama cha Democratic ametetea diplomasia akisema, ndiyo njia pekee ya kukabiliana na kadhia ya nyuklia ya Iran, na akaongezea kwa kusema: “huwezi kuufuta ujuzi kwa kuupiga mabomu hata kama utaua idadi yoyote ile ya wanasayansi”.
Mark Warner seneta mwingine wa chama cha Democratic, naye pia amewaeleza waandishi wa habari kwamba, tathmini iliyotolewa na serikali ya Trump kuhusu athari za mashambulio ya kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran kuwa ni ya “ukurupukaji”.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, kadiri muda unavyopita, ndivyo shaka inavyoongezeka kuhusu madai ya serikali ya Washington kwamba iliuangamiza kikamilifu mpango wa nyuklia wa Iran katika mashambulio ya kivamizi iliyofanya usiku wa manane wa kuamkia Jumapili ya tarehe 22 Juni dhidi ya vituo vitatu vikuu vya nyuklia vya Fordo, Natanz na Esfahan.
Kuhusiana na hilo, televisheni ya CNN na gazeti la New York Times zilifichua ripoti iliyotolewa na “Shirika la Intelijensia ya Ulinzi” la Marekani iliyoeleza kwamba, mitambo mikuu ya mpango wa nyuklia wa Iran haijaangamizwa na kwamba mashambulio hayo yamerudisha nyuma maendeleo ya nyuklia ya Iran kwa miezi michache tu, na si miaka kadhaa.
Kufuatia kufichuliwa kwa ripoti hiyo, maafisa wa serikali ya Trump walitoa kauli mbalimbali za hasira za kuzishambulia CNN na New York Times…/