Amnesty International: Israel inatumia njaa kama silaha ya vita
(last modified Thu, 03 Jul 2025 12:03:46 GMT )
Jul 03, 2025 12:03 UTC
  • Amnesty International: Israel inatumia njaa kama silaha ya vita

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani na Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International yameonya kuhusu hali mbaya ya wakazi wa Ukanda wa Gaza na kubainisha kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitumia njaa kama wenzo na silaha ya kivita.

Taarifa ya mashirika hayo ni muendelezo wa tahadhari za kimataifa ambazo zimekuwa zikitolewa zikionya kuhusu maafa ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kwamba, fursa ya kuzuia njaa huko Gaza inakaribia kumalizika kabisa, na maelfu ya familia zaidi zitafikia ukingoni mwa kuporomoka ikiwa msaada wa chakula hautawasili katika eneo hilo.

Katika upande mwingine Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limetangaza wazi kwamba, utawala wa Kizayuni unatumia njaa kama silaha ya vita kwa kuwazingira na kuwatia njaa raia.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limeonya kwamba simulizi za Wapalestina kuhusu kupokea msaada wa chakula zinaonyesha kuwepo kwa mfumo hatari wa usambazaji wakati huo huo wa ulipuaji wa mabomu na kulazimika kuyahama makazi yao.

Amnesty International pia imesisitiza kuwa, utawala unaokalia kwa mabavu umegeuza ombi la msaada wa chakula kuwa chambo na mtego wa kifo kwa Wapalestina wenye njaa.

Shirika hilo limetoa wito wa kushinikizwa mara moja utawala unaoukalia kwa mabavu Quds ukomeshe mzingiro huo na kusimamisha mauaji ya halaiki na kusisitiza ulazima wa kuwekewa vikwazo vya kijeshi, kutoa adhabu kwa maafisa wa utawala huo na kushirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.