Jeshi la Nigeria lashadidisha operesheni dhidi ya Boko Haram
(last modified Sat, 24 May 2025 07:02:45 GMT )
May 24, 2025 07:02 UTC
  • Jeshi la Nigeria lashadidisha operesheni dhidi ya Boko Haram

Jeshi la Nigeria limesema kuwa limewaangamiza wanachama 16 wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi, huku operesheni dhidi ya magaidi hao zikichachamaa.

Katika taarifa yake jana Ijumaa, msemaji wa jeshi, Onyechi Anele amesema wanajeshi hao waliwakabili magaidi hao kwa hujuma endelevu isiyo ya moja kwa moja katika eneo la Damboa, na kwamba majibizano ya risasi yalisababisha vifo vya magaidi wasiopungua 16.

"Msukumo mkuu wa shambulio hilo ulilenga Brigedi, na kusababisha kupelekwa haraka kwa msaada wa anga ili kuimarisha wanajeshi wa ardhini," Anele alisema katika taarifa siku ya Ijumaa.

Pia amethibitisha kuwa eneo la kuhifadhia silaha lilishambuliwa wakati wa makabiliano hayo, lakini lilidhibitiwa haraka.

Vile vile, Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Nigeria Nuhu Ribadu amesema wanamgambo 15,543 wameuawa kote nchini humo katika miaka miwili ya kwanza ya utawala wa Rais Bola Tinubu.

Kundi la kigaidi la Boko Haram lenye makao yake kaskazini-mashariki mwa Nigeria na ambalo pia linaendesha harakati zake katika nchi za Chad, Niger, kaskazini mwa Cameroon na Mali, limefanya mfululizo wa mashambulizi mabaya na kuwafukuza watu wasio na hatia kwa zaidi ya muongo mmoja.

Jimbo la Borno, katika miezi michache iliyopita, limeshuhudia ongezeko la shughuli za magaidi, wakitumia vilipuzi na mabomu kufanya uharibifu.