Serikali ya Kenya kusaidia familia za Waislamu wenye njaa mwezi wa Ramadhani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136502-serikali_ya_kenya_kusaidia_familia_za_waislamu_wenye_njaa_mwezi_wa_ramadhani
Serikali ya Kenya imeweka mpango wa kusaidia familia za Kiislamu zilizo katika mazingira magumu huku zikijiandaa kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhan wiki ijayo.
(last modified 2026-02-11T07:05:37+00:00 )
Feb 11, 2026 07:05 UTC
  • Rais William Ruto wa Kenya akiingia katika ukumbi wa dhifa ya Futari mwaka jana katika Ikulu jijini Nairobi
    Rais William Ruto wa Kenya akiingia katika ukumbi wa dhifa ya Futari mwaka jana katika Ikulu jijini Nairobi

Serikali ya Kenya imeweka mpango wa kusaidia familia za Kiislamu zilizo katika mazingira magumu huku zikijiandaa kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhan wiki ijayo.

Ramadhan ya mwaka huu inakuja wakati ambapo maeneo kadhaa nchini Kenya yanakabiliwa na ukame.

Baadhi ya kaunti zilizoathirika ni Mandera, Turkana, Wajir, Garissa, Marsabit, Isiolo, Kajiado, Kilifi, Kwale, Lamu na Tana River.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Wesley Koech, amenukuliwa na gazeti la Taifa Leo akisema hatua hiyo inalenga kupunguza mzigo wa kifedha kwa familia hizo wakati wa mwezi mtukufu. Amesisitiza kuwa lengo la serikali ni kuona Waislamu wakitekeleza ibada ya mfungo kwa urahisi.

Katika eneo lote la Pwani, maandalizi yanaendelea kwa kasi kuelekea Ramadhan.

Wafanyabiashara wanaongeza bidhaa madukani ili kuhakikisha waumini wanapata mahitaji yote muhimu, huku maafisa wa usalama pia wakiongeza ulinzi kutokana na shughuli nyingi zinazotarajiwa kuendelea hadi usiku wa manane na alfajiri.

Kamishna huyo wa Kaunti, ameongeza  kuwa kundi la kigaidi la Al-Shabaab huwa na mazoea ya kutekeleza mashambulizi kabla au mara tu baada ya Ramadhan kuanza. Kwa msingi huo, amesema  a vyombo vya usalama vimeimarisha doria ili kuhakikisha usalama wa umma wakati wote.

Maafisa wa usalama katika kaunti za Mombasa, Kwale na Kilifi, ambako magenge ya vijana mara nyingi huleta vurugu wakati kama huu, pia walisema wameongeza juhudi za kiusalama.

Wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi wa Ukanda wa Pwani, Bw Ali Nuno, aliwaagiza maafisa wa polisi kukabiliana vikali na wahalifu ambao hushambulia raia kwa panga.