Iran yatengeneza dawa ya kutibu saratani kwa kutumia teknolojia ya nyuklia
Iran inatarajiwa hivi karibuni kuzindua AlphaZa, dawa ya kwanza ya tiba ya nyuklia ya kutibu saratani iliyotengenezwa nchini inayotumia chembe za alfa (alpha‑emitting radiopharmaceutical), kwa ajili ya kutibu saratani zilizo katika hatua ya juu ambazo hazijaitikia tiba za kawaida.
Kwa mujibu wa Mohammad Eslami, mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI), dawa hiyo inatarajiwa kuingia sokoni hivi karibini.
Eslami amesema AlphaZa ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya Iran katika nyanja ya tiba ya nyuklia, na itapanua uwezo wa nchi hiyo katika matibabu ya saratani yanayolenga moja kwa moja seli zilizoathirika.
Dawa hiyo, ambayo imepitia miaka kadhaa ya utafiti na majaribio ya kitabibu, hutumia mbinu ya hali ya juu ya tiba lengwa ya radionuklidi. Maendeleo haya yanaifanya Iran kuwa miongoni mwa idadi ndogo ya mataifa duniani yenye teknolojia ya kutengeneza na kutumia dawa za saratani zinazotegemea chembe za alfa.
Kwa mujibu wa mkuu wa wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran , idadi ya dawa za radiopharmaceutical zinazozalishwa ndani ya Iran sasa imezidi 76, na bidhaa hizo zinasambazwa katika zaidi ya vituo 230 vya tiba kote nchini.
Eslami pia ametangaza kuwa dawa 20 mpya za aina hiyo ziko katika hatua ya utafiti na maendeleo, na zinatarajiwa kuingia katika uzalishaji ndani ya mwaka wa sasa wa Iran.
Eslami amesisitiza kuwa uzalishaji na usambazaji wa dawa za radiopharmaceutical umeendelea bila kukatizwa licha ya changamoto mbalimbali.
Aidha, amebainisha kuwa baadhi ya dawa zilizotengenezwa Iran sasa zinafikia viwango vya ubora vinavyolingana na bidhaa zinazotengenezwa katika nchi zinazoongoza katika sekta hii.
Eslami pia amesema Iran inasafirisha dawa hizo nje ya nchi, akieleza kuwa bidhaa za radiopharmaceutical za Iran tayari zimefikia masoko katika mabara matano duniani.