Iran: Hakutakuwa na makubaliano yoyote iwapo hatutorutubisha wenyewe urani
(last modified Fri, 23 May 2025 06:28:46 GMT )
May 23, 2025 06:28 UTC
  • Iran: Hakutakuwa na makubaliano yoyote iwapo hatutorutubisha wenyewe urani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa, suala la kurutubisha urani ni mstari mwekundu wa Jamhuri ya Kiislamu katika mazungumzo yajayo ya nyuklia na Marekani na kama Washington itang'ang'ani msimamo wake wa kukataa kurutubishwa urani ndani ya Iran, basi hakuna makubaliano yoyote yatakayofikiwa.

Sayyid Abbas Araghchi ambaye mapema leo Ijumaa ameelekea Rome, mji mkuu wa Italia, kwa ajili ya kushiriki duru ya tano ya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana baina ya Iran na Marekani, amesema pia kuwa, "Hatutoachana na haki zetu. Mradi wetu wa nyuklia ikiwa ni pamoja na kurutubisha urani ndani ya Iran, lazima uendelee. Lakini tuko tayari kuchukua hatua za kujenga imani." 

Amesema: "Ikiwa kile maafisa wa Marekani wanachokisema katika mahojiano yao kwamba hawaiamini Iran katika kurutubisha urani, ni kweli, basi natangaza hadharani kwamba hakutakuwa na makubaliano yoyote."

"Lakini ikiwa lengo lao ni kuhakikisha kuwa hatumiliki silaha nyuklia, makubaliano ya namna hiyo yanaweza kufikiwa kwa sababu sisi tangu zamani hatuna haja kabisa na silaha za nyuklia," amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.

Sayyid Araghchi ameongeza kuwa, Iran haijawahi kuwa na nia ya kuunda silaha ya nyuklia ingawa inao uwezo wa kiufundi wa kufanya hivyo.

Amekariri kuwa, silaha za nyuklia hazina nafasi katika mikakati ya kiulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwani kwa mujibu wa itikadi yake ya Kiislamu, ni haramu kumiliki silaha za maangamizi ya umati zikiwemo za nyuklia.

Akizungumzia vitisho vya Israel inayojilabu kuwa itashambulia vituo vya nyuklia vya Iran, Araghchi amesema, Iran iko tayari kujilinda na kwamba majibu yake yatakuwa ya haraka na ya nguvu kubwa.