Iran yaitaka Vatican ichukue hatua za haraka kukomesha mauaji ya kimbari Gaza
(last modified Sat, 24 May 2025 07:10:01 GMT )
May 24, 2025 07:10 UTC
  • Iran yaitaka Vatican ichukue hatua za haraka kukomesha mauaji ya kimbari Gaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, katika mkutano na maafisa wa Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Duniani, Vatican huko mjini Rome, ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kimataifa kukomesha uhalifu unaoendelea kufanyika Gaza, na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inafika katika eneo hilo lililozingirwa.

Araghchi ambaye alikuwa mjini Rome kuhudhuria duru ya tano ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, jana Ijumaa alikutana na Kadinali Pietro Parolin, Waziri Mkuu wa Vatican.

Askofu Mkuu Paul Gallagher, Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatican pia alihudhuria mkutano huo. Araghchi alitoa salamu za rambirambi kwa kuaga dunia Papa Francis na kupongeza kuchaguliwa kwa Papa Leo wa 14 kuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani.

Wakati wa mkutano huo, Araghchi alielezea msimamo wa Iran kuhusu matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia na kuwafahamisha maafisa wakuu wa Vatican kuhusu mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanayoendelea kati ya Iran na Marekani.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Italia wamefanya mazungumzo kwa njia ya simu

Wakati huo huo, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Italia katika mazungumzo yao kwa njia ya simu wamezungumzia matukio ya hivi punde katika eneo la Magharibi mwa Asia hususan kuendelea mauaji ya kimbari huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na kusisitiza juu ya haja ya kuchukuliwa hatua za dharura za kukomesha mauaji hayo na kutoa msaada kwa watu waliokimbia makazi yao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambaye ameenda Rome kushiriki duru ya tano ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya Iran na Marekani, alipokea simu kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Antonio Tajani, ambaye yuko nje ya nchi, na kumjulisha kuhusu matokeo ya mazungumzo hayo ya Ijumaa.