Iran yawakamata magaidi wa Mossad kaskazini magharibi mwa nchi
Vikosi vya usalama vya Iran vimewakamata magaidi wawili wa shirika la ujasusi la Mossad la utawala haramu wa Israel kaskazini magharibi mwa Iran.
Kamandi Polisi ya Iran ilitangaza Jumamosi kuwa maafisa hao wawili wa Mossad walikamatwa katika Kaunti ya Savojbolagh mkoani Alborz, kaskazini magharibi mwa Iran.
Taarifa hiyo imesema: "Kupitia juhudi za polisi wa mkoa wa Alborz, wanachama wawili wa kundi la kigaidi linalofungamana na Mossad walikamatwa."
Taarifa hiyo imebaini kuwa magaidi hao walikuwa wakitengeneza mabomu, vilipuzi, mitego iliyotegwa, na vifaa vya kielektroniki katika nyumba moja ya kundi hilo.
Shirika la kijasusi na kigaidi la Mossad husimmia shughuli za kijasusi na operesheni za siri nje ya mipaka ya utawala haramu wa Israel.
Maafisa wa usalama wa Iran wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba Wairani wako macho dhidi ya adui Muisraeli ambaye amekuwa akifanya juhudi kubwa za kudhuru taifa la Iran katika miongo kadhaa iliyopita.
Ijumaa asubuhi, utawala wa Israel ulianzisha uchokozi mpya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, safari hii ukisababisha kuuawa kwa makamanda kadhaa wakuu wa jeshi la Iran na wanasayansi wa nyuklia, pamoja na kuwaua raia wengi, wakiwemo wanawake na watoto.
Katika kujibu uchokozi wa Israel, Iran imetekeleza mashambulizi makubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani katika maeneo yanayokaliwa Ijumaa na Jumamosi, ikiwa ni hatua ya kujihami.
Mashambulizi ya Iran yaliwalenga maeneo ya viwanda vya kijeshi katika miji kama vile mji mkuu Tel Aviv, jiji la bandari linalokaliwa la Haifa, n.k.