Araghchi: Iran iko tayari kukabiliana na tishio au uovu wowote
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa jeshi la Iran liko katika hali ya utayari kamili kulinda mamlaka na heshima ya taifa dhidi ya tishio au uchokozi wa aina yoyote.
Seyyed Abbas Araghchi, amesisitiza kuwa chanzo na sababu kuu ya hali ya kutotulia katika ukanda wa Ghuba ya Uajemi na Mlango wa Bahari wa Hormuz ni uchokozi wa kijeshi unaoilenga Iran, hasa ulioanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni.
Kauli hii ilitolewa katika mazungumzo ya simu kati ya Araghchi na mawaziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Qatar, Saudi Arabia, Misri, Iraq na Jamhuri ya Azerbaijan, ambapo walijadili mwelekeo wa kisiasa na matukio ya sasa ya eneo hilo.
Bw. Araghchi aliwaeleza wenzake kuhusu msimamo na hatua za kidiplomasia zinazochukuliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa lengo la kukomesha vita vinavyolazimishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran, na kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo.
Alikumbusha kwamba uvamizi wa kijeshi wa Marekani na washirika wake wa Kizayuni ndio chanzo cha ukosefu wa amani katika Ghuba ya Uajemi na Mlango wa Bahari wa Hormuz. Araghchi ameongeza kuwa Iran, kwa nia njema na uwajibikaji, imekubali kuingia katika duru mpya ya mazungumzo kupitia upatanishi wa Pakistan, licha ya kutokuwa na imani na upande wa Marekani kutokana na historia ya ahadi zilizovunjwa mara kwa mara.
Aidha, Araghchi ameyashukuru mataifa ya eneo yanayojitahidi kuendeleza njia za kidiplomasia na kulinda eneo lisije likakumbwa na athari hatari za uvamizi wa kijeshi wa mara nyingine. Amesisitiza kuwa Iran haikuanza vita hivi; na ingawa inabaki wazi kwa mazungumzo iwapo Marekani itabadilisha mwelekeo wake wa vitisho na matendo ya uchokozi, vikosi vya ulinzi vya Iran bado viko macho, vikiwa tayari kulinda taifa kwa uthabiti na ukamilifu dhidi ya tishio lolote au nia mbaya.
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo za eneo nao walieleza msimamo wa serikali zao katika kusaidia diplomasia na suluhisho za amani za kumaliza vita na kutatua tofauti, wakionyesha utayari wao kushiriki katika mchakato huu wa kutafuta utulivu wa ukanda wa Asia Magharibi.