Israel yapewa kichapo Lebanon, wanajeshi wasiopungua 2 wauawa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i138092-israel_yapewa_kichapo_lebanon_wanajeshi_wasiopungua_2_wauawa
Wanajeshi wasiopungua wawili wa Israel wameuawa na wengine zaidi ya 27 kujeruhiwa katika mashambulizi kadhaa ya ndege zisizo na rubani za harakati ya Hizbullah kusini mwa Lebanon, huku Israel ikiitonya Washington kwamba uwezo wake wa kukabiliana na harakati ya mapambano ya Lebanon unakaribia kusambaratika.
(last modified 2026-05-02T07:21:03+00:00 )
May 02, 2026 07:19 UTC
  • Mpiganaji wa Hizbullah
    Mpiganaji wa Hizbullah

Wanajeshi wasiopungua wawili wa Israel wameuawa na wengine zaidi ya 27 kujeruhiwa katika mashambulizi kadhaa ya ndege zisizo na rubani za harakati ya Hizbullah kusini mwa Lebanon, huku Israel ikiitonya Washington kwamba uwezo wake wa kukabiliana na harakati ya mapambano ya Lebanon unakaribia kusambaratika.

Duru za Israel zimethibitisha kuwa mwanajeshi mmoja aliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati Hizbullah iliposhambulia kundi la wanajeshi wa utawala huo kwa kutumia ndege isiyo na rubani kusini mwa Lebanon siku ya Alhamisi, na kuongeza kuwa wawili kati ya waliojeruhiwa walikuwa katika hali mbaya.

Kwa mujibu wa ripoti hizo, huyo anakuwa mwanajeshi wa tatu wa Israel kuuawa na ndege zisizo na rubani za Hizbullah kusini mwa Lebanon katika siku kadhaa za karibuni.

Katika tukio tofauti, vyanzo vya Israel vimekiri kuwa mwanajeshi mwingine ameuawa na wengine 15 kujeruhiwa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Hizbullah siku ya Alhamisi. Vyombo vya habari vya Israel vimewanukuu wachambuzi wakisema kwamba siku ya Alhamisi ilikuwa "siku nyingine ngumu" kwa wanajeshi wa Israel katika upande wa kaskazini.

Mapema siku ya Alhamisi, vyanzo vya habari vya Israel vilikiri kwamba wanajeshi 12 wa utawala huo walijeruhiwa katika shambulio la Hizbullah kwa kutumia ndege isiyo na rubani iliyolenga mkusanyiko wa wanajeshi waliojihami katika mji wa Shomera Magharibi mwa Galilaya.

Hizbullah ilitangaza kuwa imeshambulia vifaru viwili vya Merkava katika mji wa Bint Jbeil kwa kutumia ndege zisizo na rubani.

Katika muktadha huo, vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa utawala wa Tel Aviv umeifahamisha rasmi serikali ya Marekani kwamba uwezo wake wa kukabiliana na Hizbullah unakaribia kuporomoka.