Uwezo mkubwa wa Iran wa kutoa pigo kali kwa utawala wa Kizayuni
Ukiwa unatekeleza mpango wa pamoja na Marekani chini ya taa ya kijani ya Washington, baada ya vitisho vya mara kwa mara vya kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran, hatimaye utawala wa Kizayuni umeanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya shabaha mbalimbali nchini Iran alfajiri ya Ijumaa, Juni 13, ambayo yamepelekea kuuawa shahidi idadi kadhaa ya makamanda wakuu wa kijeshi na raia wa kawaida, wakiwemo wanawake na watoto.
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel amedai katika taarifa baada ya kuanza mashambulizi hayo kuwa lengo ni kuharibu miundombinu ya nyuklia na makombora ya Iran.
Iran imesisitiza mara kwa mara katika kujibu vitisho vya Tel Aviv kwamba itatoa jibu kali na la kuumiza kwa chokochoko zozote za Israel.
Hili linaweza kutoa pigo kali kwa Israel, kwa kuzingatia uwezo mkubwa wa makombora na ndege zisizo na rubani za Iran, pamoja na mbinu bora za kivita ambazo majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu yamekuwa yakizitumia katika uwanja huu kwa miaka mingi.
Baada ya utawala wa Kizayuni kuishambulia Iran, Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza katika ujumbe kwamba, utawala wa Kizayuni utarajie adhabu kali.
Kamandi Kuu ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imetangaza katika taarifa yake kwamba, jibu la Iran kwa utawala wa Kizayuni litakuwa kali na la kujutisha.
Iran sasa iko katika kiwango cha juu zaidi cha utayari wa kijeshi, na jibu lake kwa hakika litaishtua Israel. Wakati huo huo, kufichuliwa matokeo ya operesheni kuu ya kiintelijensia ya Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni kumeipa Iran fursa kubwa ya kijasusi kuhusu shabaha za Marekani na Kizayuni, na Iran hivi sasa inaweza kuwashangaza maadui zake kwa kutoa mapigo ya kuhilikisha kabla ya maadui kuchukua hatua yoyote.
Kwa kuzingatia eneo dogo la utawala wa Kizayuni, kasoro za kimkakati na msongamano mkubwa wa watu, bandari, vituo vya umma, viwanda, vya uzalishaji, kambi za kijeshi na vituo vya anga, pamoja na vifaa vya nyuklia, utawala huu kwa kawaida una shabaha nyingi zinazoweza kulengwa kirahisi na jeshi la Iran. Ni wazi kuwa maeneo hayo yanaweza kulengwa na kuisababishia Israel mapigo mazito na makali ya kijeshi kwa kutumia ndege zisizo na rubani za kujitoa mhanga zenye uwezo wa kuruka umbali wa kilomita 2,000 na aina mbalimbali za makombora ya balistiki ambayo yanaweza kufika Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh, Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alitangaza tarehe 11 Juni kwamba katika mafanikio ya hivi karibuni ya Iran ni kombora la kichwa chenye uzito wa tani 2, ambalo lilifanyiwa majaribio wiki moja iliyopita.
Kombora hili ni toleo la hivi karibuni zaidi la familia ya kombora la Khorramshahr na ni aina ya kombora lisilohitaji kuongozwa hatua kwa hatua katika awamu yake ya mwisho ya kulenga shabaha.
Khorramshahr-4 (Khyber) ni kombora la masafa marefu ya kilomita 2,000. Kichwa chake cha kivita kina uzito wa zaidi ya kilo 1,800, na kasi yake ndani ya angahewa ni takriban Mach 8 na nje ya angahewa ni hadi Mach 16.
Kichwa cha kombora hili, chenye urefu wa takriban mita 4, ni mojawapo ya vichwa vya kivita vikubwa na bora zaidi kuwahi kutengenezwa, vyenye uwezo wa kubeba zaidi ya tani moja ya mabomu.
Kombora la Khyber-Shakan, lenye masafa ya kilomita 1,450, lina usanidi wa vichwa vitatu vya vita, ambavyo hutumika kudumisha uthabiti wa vichwa vya vita wakati wa maneva nzito.
Suala jingine katika kuchunguza kombora la Khyber-Shakan ni aina ya mlipuko wa vichwa vya vita. Kulingana na picha zilizochapishwa, kichwa cha vita kina aina ya mlipuko wa hali ya juu, lakini kwa mujibu wa kamanda wa Kikosi cha Wanaanga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, nyenzo zimetumika katika vichwa vya vita vya Khyber-Shakan ambavyo vimeongeza nguvu zake za kulipuka hadi mara kadhaa za TNT.
Kombora la "Fattah 1" la hypersonic limetengenezwa na wataalamu wa Jeshi la Wanaanga la IRGC.
Kombora hili pamoja na uwezo wake wa kimbinu, lina uwezo wa kufikia kasi ya juu sana na kufanya harakati mbalimbali ndani na nje ya angahewa ya dunia ili kukwepa mifumo mbalimbali ya ulinzi wa anga ya adui kutokana na hatua yake ya pili ya kutumia mafuta na kuhamishika.
Sifa zingine za kombora hili ni pamoja na: mafuta ya hatua ya 2, umbali wa kilomita 1,400, harakati zisizotabirika ndani na nje ya angahewa ya dunia, kasi ya juu ya Mach 25 nje ya angahewa na kasi ya papo kwa hapo ya Mach 13 hadi 15, matumizi ya misombo ya aloi ambayo hunyonya safu ya chini ya ulinzi wa rada.
Sifa bainifu za kombora la Fatah 1 hypersonic ni pamoja na kuongezeka kwa usahihi wa kulenga shabaha, kasi ya juu sana, harakati za kushangaza za kukwepa adui na uwezo wa kujificha na kupita mifumo ya rada.
Kombora la Fatah 2 la hypersonic lina uwezo wa kuruka na kusafiri kwa kasi kubwa, na limeainishwa katika kitengo cha glider za hypersonic (HGV).
Ni nchi nne pekee duniani, ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ndizo zinamiliki teknolojia ya aina hii ya silaha za hypersonic.
Badala ya kupata mwinuko kama makombora ya balestiki, makombora ya HGV kama vile Fatah 2 husafiri kwa mwinuko wa chini zaidi kukiwa na uwezekano wa kubadilisha mkondo kuelekea lengo, na kufanya iwe vigumu kwa rada za tahadhari za adui kuyagundua.

Makombora mengine ya kisasa ya Iran ni pamoja na "Emad" lenye masafa ya kilomita 1,700, "Qadr H" lenye masafa ya kilomita 1,650, "Qadr F" lenye masafa ya kilomita 1,950, "Qiyam" lenye masafa ya kilomita 800, Haj Qassem lenye masafa ya kilomita 1,400, "Sijjil" lenye umbali wa kilomita 2,000, na kombora la "Paveh" lenye masafa ya kilomita 1,650.
Nukta ya mwisho ni kwamba, uwezo wa kiulinzi na uzuiaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran una vipengele kadhaa, mojawapo ikiwa ni uwezo wa makombora yake, kiasi kwamba Iran ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani katika uwanja huu.
Kwa upande mwingine, ndege zisizo na rubani za Iran zenye uwezo wa kuruka katika miinuko ya juu, kukaa angani kwa muda mrefu, na kubeba aina mbalimbali za silaha, zina nafasi muhimu katika kuliongezea jeshi hilo uwezo wa kiupelelezi na kioperesheni.
Maendeleo haya, pamoja na ustawi wa mifumo ya ulinzi na teknolojia mpya za kivita vya kielektroniki, yameifanya Iran itambulike kama mojawapo ya wadhamini wakuu wa usalama na masuala ya kijeshi katika Asia Magharibi na hivyo kubuni kizuizi kikubwa dhidi ya vitisho vya kieneo na kimataifa. Jamhuri ya Kiislamu hivi karibuni pia imeonyesha nguvu kubwa katika masuala ya usalama na intelijensia. Uhamisho usio na mfano wake wa idadi kubwa ya nyaraka za siri kutoka utawala wa Kizayuni katika nyanja za nyuklia, kijeshi, kiusalama n.k, unaashiria uimarikaji mkubwa wa shughuli za intelijensia za Iran, jambo ambalo linaonyesha kuwa mbali na uga wa makombora, Iran pia ndiyo nchi inayoongoza katika eneo hili katika masuala ya intelijensia.