Jenerali Hatami ateuliwa kuwa Kamanda mpya wa Majeshi ya Iran
Brigedia Jenerali Amir Hatami ameteuliwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, kuwa Kamanda Mkuu mpya wa Majeshi ya Iran.
Katika dikrii ya jana Ijumaa, Ayatullah Khamenei, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran, amempandisha cheo Brigedia Jenerali Hatami hadi cheo cha Meja Jenerali, na kumteua kuwa Mkuu mpya wa Jeshi la Iran.
"Kwa kuzingatia hifadhi kubwa ya rasilimali watu wenye uwezo na waaminifu ndani ya Jeshi (la Iran), pamoja na uzoefu uliopatikana wakati wa Vita vya Kujihami Kutakatifu na zaidi, inatarajiwa kwamba wakati wa uongozi wako - kwa muelekeo wa mageuzi na mapinduzi - kutashuhudiwa uboreshaji wa utayari wa makabaliano, umakini wa kiroho na kiitikadi, utimilifu wa mahitaji ya wafanyikazi, na mshikamano na vikosi vingine vya jeshi," amesema Kiongozi Muadhamu.
Jenerali Hatami alihudumu kama Waziri wa Ulinzi wa Iran kutoka mwaka 2017 hadi 2021. Anachukua nafasi ya Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi, ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu mpya wa Majeshi ya Iran mapema jana.
Kufuatia mashambulizi ya utawala Israel, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameteua wakuu wapya wa kijeshi katika nyadhifa kuu, akisisitiza kuendelea nguvu za kiroho ndani ya Vikosi vya Wanajeshi wa Iran.
Aidha Kiongozi Muadhamu ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Iran amemteua Luteni Jenerali Ali Shadmani kuwa Kamanda wa makao makuu ya Kikosi cha Khatam al-Anbiya, akichukua nafasi ya Meja Jenerali Gholam Ali Rashid, aliyeuawa shahidi pia katika mashambulio ya Israel dhidi ya Iran.
Wakati huo huo, Ayatullah Khamenei amemteua Luteni Jenerali Mohammad Pakpour kuwa mkuu mpya wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) akichukua nafasi ya kamanda shujaa aliyeuawa shahidi pia na Wazayuni, Luteni Jenerali Hossein Salami.