"Iwapo maadui wangeliamini Iran inaweza kushindwa, wasingejadiliana"
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amesisitiza kuwa, jukumu la msingi la wizara hiyo ni kujitahidi kuondosha vikwazo na kuongeza kuwa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayesimamia Diplomasia ya Kiuchumi na balozi za Iran nje ya nchi zinapaswa kuwezesha mchakato huo na kuondolewa vikwazo vyote dhidi ya taifa hili.
Akizungumza katika kongamano la diplomasia ya uchumi lililohudhuriwa na wafanyabiashara wa Iran huko Shiraz, kusini mwa Iran jana Alkhamisi, Araghchi alisema diplomasia ina kanuni mbili za kimsingi: ujirani mwema, na diplomasia ya kiuchumi.
Ameleza bayana kuwa, Iran kwa muda mrefu imekuwa ikifuata diplomasia ya ujirani mwema, huku diplomasia ya pili ikihusisha Wizara ya Mambo ya Nje kuwezesha fursa za kibiashara badala ya kujihusisha na biashara moja kwa moja.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, biashara za Iran zinazokwepa vikwazo zimeweza kuipa motisha timu ya mazungumzo ya Jamhuri ya Kiislamu, na kuwakatisha tamaa wale wanaotekeleza vikwazo hivyo.
"Iwapo adui angekuwa na uhakika kwamba Iran inaweza kupigishwa magoti, asingeingia katika mazungumzo hata kidogo," amesema Araghchi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, diplomasia ya kiuchumi inakwenda zaidi ya shughuli za kifedha; ni kuhusu kuunda njia kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kujihusisha na masoko ya nje.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amebainisha kuwa, kwa kupunguza athari za vikwazo, Tehran inalenga kuyafinyanga mazungumzo na nchi za Magharibi na kuunda fursa mpya za ushiriki wa kiuchumi. Haya yanajiri huku duru ya tano ya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani ikitazamiwa kufanyika leo Ijumaa nchini Italia.