Sayyid Hashem Safiyyuddin, Mjenga Hamasa ya Muqawama Itakayodumu Milele
SalamuLlahi Alaykum wapenzi wasikilizaji, na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba wa kuuawa shahidi Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon, Sayyid Hashem Safiyyuddin.
Ni kweli, kwamba hii leo, na kidhahiri, viongozi wa Hizbullah kama Sayyid Hassan Nasrullah na Sayyid Hashem Safiyyuddin hawako pamoja tena na harakati hiyo, lakini roho zao na uongozi wao ungali uko kwenye medani ya mapambano na unaendelea kuilinda Lebanon na wananchi wake wasio na ulinzi.
Sayyid Hashem Safiyyuddin alizaliwa mwaka 1964 katika mji wa Deir Qanoun En Nahr kusini mwa Lebanon katika ukoo mashuhuri wa Waislamu wa Kishia. Ukoo wa Safiyyuddin ulikuwa ukitajika sana katika uga wa kisiasa na kidini; na maulamaa wengi wa Kishia na wanasiasa mashuhuri wa Kishia wa nchini Lebanon, aghalabu yao wametokea kwenye ukoo huo.
Katika muongo wa 1980, Sayyid Hashem Safiyyuddin alielekea Hawza, yaani vyuo vya kidini, vya Iraq na Iran kwa ajili ya kuendelea na masomo. Wakati akiwa masomoni katika mji wa Qom nchini Iran, Safiyyuddin alivutiwa na fikra za kisiasa za Imamu Khomeini (RA) na akawa mmoja wa wafuasi wake wakubwa. Katika moja ya maandiko yake, ameashiria nafasi ya umoja na kuwa kitu kimoja katika kuwezesha kupatikana mafanikio na ushindi kwenye harakati na mavuguvugu ya Kiislamu na kulielezea hilo kuwa ndiyo njia ya kuishinda mifarakano.
Mwaka 1994, harakati ya Hizbullah ilimtaka Sayyid Hashem Safiyyuddin ahitimishe shughuli zake za masomo katika chuo kikuu cha kidini cha Qom na kurudi Lebanon kwa ajili ya kushika nyadhifa na masuulia muhimu katika harakati hiyo.
Sayyid Hashem Safiyyuddin na Sayyid Hassan Nasrullah pamoja na Imad Mughniyah, maarufu kwa lakabu ya Haj Ridhwan, walijenga "mihimili mitatu ya nguvu" za Hizbullah, ambapo Imad alitambulika kama mhimili mkuu wa nguvukazi ya kijeshi; Sayyid Nasrullah, mhimili wa nguvukazi ya kisiasa na Sayyid Hashem, wa nguvukazi ya kiidara na uendeshaji. Miaka kadhaa baadaye, mnamo Oktoba 2008, Sayyid Hashem Safiyyuddin alichaguliwa kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo ya Muqawama ya Lebanon.
Kikosi cha Ridhwan ndicho kikosi mashuhuri zaidi na chenye wapiganaji stadi na hatari zaidi wa Hizbullah, ambao jukumu muhimu zaidi walilokabidhiwa wapiganaji hao, ni kujiweka tayari kuingia kwenye ardhi ya Palestina katika mapigano yoyote tarajiwa yatakayotokea katika siku za usoni. Miezi michache kabla ya kuanza Operesheni ya Kimbunga au Gharika ya Al-Aqsa, kikosi maalumu cha Ridhwan, ambacho ni kikosikazi cha wapiganaji maalumu wa Hizbullah ya Lebanon kilifanya mazoezi ya kijeshi, ambayo yaliakisiwa sana katika duru za vyombo vya habari na hasahasa vyombo vya habari vya Kizayuni. Katika manuva hayo, wapiganaji wa kikosi cha Ridhwan waliokuwa wamebeba silaha za kisasa, walionekana wakipanda ukuta unaofanana na uzio uliowekwa na utawala wa Kizayuni.
Alon Ben-David, mwandishi wa habari wa masuala ya kijeshi wa Chaneli ya 13 ya Israel, ambaye ametabahari katika masuala ya kiulinzi na kijeshi, anasema hivi kuhusu luteka hiyo: "kikosi maalumu cha Ridhwani kinaundwa na wapiganaji elfu nane wa nchi kavu waliopewa mafunzo maalumu, ambao baada ya kutolewa amri maalumu ya kijeshi, wanaweza ndani ya muda wa saa chache tu, kuvuka mpaka na kukiteka kitongoji cha Israel. Kisha baada ya hapo hufuatiwa na kundi la msururu mkubwa wa maroketi na makombora linalotoa msukumo na msaada kwa kikosi hicho".
Kuzawadiwa silaha ya Shahidi Imad Mughniyah kwa kamanda wa kikosi maalumu cha Ridhwan, ni moja ya matukio yaliyoakisiwa kwa wingi kwenye vyombo rasmi vya habari na mitandao ya kijamii. Shahidi Hashem Safiyyuddin, Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah alisema yafuatayo katika mahojiano aliyofanya baada ya manuva hayo: "asubuhi, kabla ya kuanza manuva, familia ya Haj Imad Mughniyah ilikuja kwenye eneo la mazoezi; na mwana wa Haj Imad, akazungumza kwa niaba ya familia na akasema: 'sisi tunataka kuitoa silaha yake binafsi na kukitunukia kikosi cha Ridhwan". Silaha hiyo ingeliweza kuhifadhiwa ikabaki kuwa kumbukumbu kwa Imad mdogo, yaani mjukuu wa Haj Imad, ingeliweza kubaki kwenye familia yake ikawa mirathi yake ya kiutu na kihisia, lakini familia ya Haj Imad, kama alivyokuwa yeye mwenyewe, ni ya watu wenye ukarimu na moyo wa kujitolea; na kwa hatua yao ya kukitunukia silaha yake kikosi maalumu cha Ridhwan, imetaka kueleza kwamba, chochote kile cha Haj Imad kipo kwa ajili ya kuutumikia Muqawama na kikosi cha Ridhwan. Mimi ninayo imani kwamba, iko siku kikosi maalumu cha Ridhwan kitaingia Palestina, na silaha ambayo familia ya Haj Imad imekitunukia kikosi hicho kwa ukarimu na uadhamu itaingia mkononi mwa mtu ambaye hataingia Palestina tu, bali atafika na kuingia pia Baitul Muqaddas (Jerusalem)".
Baada ya mwaka 2000 na kupatikana ushindi wa kwanza wa Hizbullah ya Lebanon, Muqawama haukujipa mapumziko hata ya dakika moja bali uliendelea kujizatiti na kujiweka kwenye utayarifu muda wote. Siku ya pili baada ya ushindi wa mwaka 2000, yalianza maandalizi ya vita vilivyofuatia, mpaka ukawadia mwaka 2006. Baada ya Vita vya Julai vilivyochukua muda wa siku 33, Imad Mughniyah alisisitiza tena kwamba "suala la kupumzika halipo asilani, tujiandaeni na kujiweka tayari kwa vita vijavyo".
Muqawama wa Kiislamu wapenzi wasikilizaji, unaielewa barabara dhati, khulka na utambulisho halisi wa adui yake; na una imani, uthabiti, uongozi wenye hekima na ushujaa na wananchi imara na wenye istiqama. Kuwa na sifa zote hizi, kunaufanya muda wote uwe katika hali ya kujiandaa na kujiweka tayari, kupiga hatua zaidi na kuendeleza njia ya mapambano na Muqawama. Kwa mtazamo wa wapiganaji wa Muqawama, mapambano na Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu ni neema itokayo kwake Yeye Allah; na Jihadi ni mlango mmoja kati ya milango ya Peponi, ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu amewafungulia mawalii wake, vipenzi vyake na waja wake makhsusi.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano aliyofanyiwa baada ya kumalizika kwa mafanikio manuva ya kikosi maalumu cha Ridhwan, Sayyid Hashem Safiyyuddin alisema: "watu wanaoifahamu jamii ya Israel wanajua kwamba, jamii hiyo haijashikana, haijaungana na wala haiko kitu kimoja. Walikuwa wakijaribu kuwaonyesha watu kuwa wako hivyo, ilhali hiyo ni jamii iliyojengwa kwa msingi wa tofauti za ndani, kufanyiana njama, mauaji na umwagaji damu. Wao hawawezi kuishi bila kufanya njama; wanafanyiana njama wao kwa wao; na ikiwa mtu ataingia kwenye jamii ya Israel, atabaini kwa uwazi kabisa kwamba kuna mambo yanayozusha tofauti baina yao; na wao wenyewe wanasema: wakati myahudi anapomuua myahudi mwenzake, huwa ndio mwisho wa dunia. Sasa hivi wanapita kwenye njia hiyo. Ukweli wa mambo ni kuwa, jamii ya Israel, imemomonyoka kwa ndani; kuna taassubi na ubaguzi wa aina mbalimbali baina yao, ambao hauwezi kufumbiwa macho kirahisi; hapo kabla walikuwa wakijaribu kufifilisha taassubi na ubaguzi huo kwa sababu ya nguvu zao za kidhahiri; lakini leo hii, ambapo wameshakuwa dhaifu kisiasa na kiusalama, hakika yao imefichuka na tofauti zao zimedhihirika.
Sisi tumeeleza kila mara kwamba, nguvu za Israel hazitokani na uwezo wake, bali zinatokana na udhaifu wa Waarabu na Waislamu. Wakati Waarabu na Waislamu walipoonyesha nguvu na uwezo wao kwa njia ya Muqawama na kudhihirisha umoja na mshikamano wao, waliidhoofisha Israel na kuanza kuyadhihirisha mambo yanayoakisi udhaifu wake. Wakati Muqawama ulipopata nguvu, dhati halisi ya Israel ilifichuka na udhaifu wa utawala huo ukadhihirika.
Sambamba na kuanza kwa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon, nayo pia iliingia kwenye medani ya mapambano ili kuuhami na kuusaidia Muqawama wa Palestina na Piganio lake Tukufu la kuikomboa Quds. Tangu yalipoanza mapigano ya Kimbunga cha Al-Aqsa, Shahidi Safiyyuddin alikuwa na nafasi na mchango muhimu katika kuwasaidia wananchi madhulumu wa Palestina; na kila mara alikuwa akisisitiza kwamba, Waislamu wote na watetezi wote wa uhuru duniani wana wajibu wa kuwatetea Wapalestina wanaonyongeshwa na kudhulumiwa, na wana jukumu la kupambana na utawala vamizi na ghasibu wa Kizayuni.
Katika aya ya 81 ya Suratul-Israa Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: "Na sema: Haki imekuja, na batili imetoweka. Hakika batili lazima itoweke!" Sayyid Hashem aliifasiri aya hii kama ifuatavyo: batili kwa dhati yake ni yenye kuelekea kutoweka, kudhoofika na kumomonyoka, lakini ili ifutike moja kwa moja inahitajika kupata nguvu haki. Leo Marekani ina hali dhaifu duniani. Udhaifu huu hauhusu eneo letu sisi tu." Kuhusiana na nukta hii, Sayyid Hashem anaashiria maandiko ya watafiti na wahakiki wengi wa Kimarekani, ambao waliyaandika hayo tangu miaka 20 hadi 25 nyuma. Watafiti hao wanasisitiza kwamba, kuna wakati Marekani ilifikia kilele cha nguvu na uwezo, na sasa hivi ni wakati wa kufifia nguvu hizo. Kipigo kikubwa cha kwanza na cha kihistoria ilichopata Marekani kiliikumba Lebanon na katika vita vile vya siku 33. Wakati chama cha Republican cha wenye misimamo mikali nchini Marekani kilipoidhibiti Iraq na Afghanistan kiliamua kulibadilisha eneo la Mashariki ya Kati; na Condoleezza Rice, mwanasiasa wa chama hicho na waziri wa mambo ya nje wa wakati huo wa Marekani ndiye aliyezungumzia suala hilo; lakini kutokana na ushindi uliopata Muqawama dhidi ya Marekani, mpango huo uligonga mwamba na hivyo ndivyo kulivyoanza kudhoofika kwa Marekani.
Katika mahojiano hayo, Sayyed Hashem Safiyyuddin alitabiri kufifia kwa nguvu za Marekani na akasema, imesalia miaka miwili tu au mitatu kabla ya kumalizika nguvu za dola hilo. Kwa mtazamo wake yeye, vita kwa tafsiri na maana yake ya jadi na inayotambulika vilimalizika kwa manufaa ya Muqawama, lakini inapasa kuendelea kuwa ngangari na imara, kwa sababu wakati ukoloni wa Kimarekani utakapotaka kuondoka katika eneo, hapana shaka yoyote utaliripua na kulivuruga.
Tangu wakati huo umepita zaidi ya mwaka mmoja huku mageuzi na mabadiliko yakiendelea kujiri katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Ulimwengu wa Waarabu, ambayo yote yanatilia nguvu hoja ya kudhoofika Marekani.
Kufuatia kuuawa shahidi Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah Ijumaa ya tarehe 27 Septemba, wachambuzi na vyombo mbalimbali vya habari vilieleza katika tathmini zao kwamba, kuna uwezekano mkubwa Sayyid Hashem Safiyyuddin atachaguliwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa Hizbullah. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nje, Safiyyuddin alishabihiana sana na Sayyid Hassan Nasrullah kwa umbo na sura na hata tabia. Lakini kwa kuzingatia pia misimamo yake mikali katika suala la uadui dhidi ya Israel na Magharibi, Wazayuni walikuwa wameshatabiri kuwa chini ya uongozi wa Safiyyuddin, muelekeo wa Hizbullah utakuwa wa msimamo mkali zaidi kuliko wa hapo awali. Suala kwamba Sayyid Hashem Safiyyuddin ndiye atakayeshika hatamu za uongozi wa Hizbullah liliwatia kiwewe viongozi wa utawala wa Kizayuni, na hatimaye mnamo tarehe 4 Oktoba, zikiwa zimepita siku sita tu tangu ulipofanya mauaji ya kigaidi na kumuua shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, utawala wa Kizayuni ulifanya shambulio jengine la kinyama na la ukiukaji sheria kwenye jengo moja katika eneo la Adh-Dhaahiya mjini Beirut, na kumuua shahidi Sayyid Hashem Safiyyuddin, Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah, shakhsia mashuhuri na mwanazuoni kipenzi cha wananchi wa Lebanon na Waislamu wote watetezi wa uhuru na ukombozi duniani.
Pamoja na hayo, kinachopasa kuzingatiwa zaidi ni kwamba, leo hii Hizbullah si harakati inayotegemea kiongozi tu, bali imesimama juu ya mhimili imara wa "kifikra" na kubadilika kuwa "taasisi iliyokita mizizi", kama alivyoeleza Imamu Khamenei katika salamu zake za rambirambi ya kwamba: "Hizbullah iko hai na inaendelea kumea, na kutekeleza jukumu na nafasi yake ya kihistoria".
Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/