Palestina yataka uingiliaji kati wa walimwengu kusitisha mashambulizi ya Israel
-
Palestina yataka uingiliaji kati wa walimwengu kusitisha mashambulizi ya Israel
Mamlaka ya Ndani ya Palestina, imetoa radiamali kwa uamuzi wa baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu kutaifisha ardhi za Ukingo wa Magharibi na kuitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua kuhusu suala hilo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Palestina “Wafa”, Ofisi ya Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeonya katika taarifa yake kuhusu hatari za uamuzi haramu wa utawala wa Kizayuni wa kubadilisha ardhi za Ukingo wa Magharibi kuwa kile kinachoitwa “ardhi za serikali” zinazodaiwa kumilikiwa na utawala huo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, uamuzi huo ni tishio kwa uthabiti na usalama, ni hatua hatari na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Imeongeza kuwa uamuzi huo usiokubalika wa “Israei” ni sawa na kuunganisha kwa vitendo ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, ni tangazo la kuanza utekelezaji wa mipango ya kuunganisha ardhi za Palestina kwa lengo la kuhalalisha ukaliaji mabavu kwa njia ya vitongoji haramu vya walowezi, na pia kumaliza makubaliano yaliyosainiwa. Aidha, unakinzana waziwazi na maazimio ya Baraza la Usalama, hasa Azimio 2334, ambalo linatangaza kuwa ujenzi wa makazi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, ikiwemo Baytul-Muqaddas Mashariki, ni haramu.
Pia Mamlaka ya Ndani ilitoa wito kwa jamii ya kimataifa, likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na serikali ya Marekani, kuingilia kati haraka ili kusitisha hatua hizi hatari za utawala wa Israel na kuulazimisha kuzingatia sheria za kimataifa, kutekeleza usitishaji mapigano na kukomesha kuongezeka kwa mvutano.