Araghchi: Iran inaunga mkono umoja wa kitaifa wa Lebanon
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imeiunga mkono na itaendelea kuinga mkono Lebanon, umoja wa kitaifa, uhuru na mamlaka ya kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu.
Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema hayo jana Alkhamisi alipolitembelea kaburi la Sayyid Hassan Nasrullah, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku akitoa mwito kwa utawala ghasibu wa Israel kuondoka katika ardhi uliozikaliwa kwa mabavu zikiwemo za Lebanon, ameeleza bayana kuwa, "Serikali na taifa la Iran linatuma salamu kwa wapambanaji wa njia ya haki, uadilifu na Muqawama, na wale ambao waliyatoa muhanga maisha yao ili kunyunyiza maji kwenye njia hii tukufu na kufungua njia ya ushindi."
Amesisitizia haja ya kupanuliwa uhusiano wa pande mbili wa mataifa mawili rafiki ya Iran na Lebanon katika nyuga zote. Sayyid Araghchi amekutana na maafisa wa serikali ya Lebanon akiwemo Waziri wa Uchumi wa nchi hiyo, ambapo amelaani chokochoko za Wazayuni dhidi ya taifa hilo la Kiarabu.
Hivi karibuni, Esmaeil Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alilaani vikali mashambulizi ya anga ya Wazayuni yaliyolenga miundombinu ya makazi, viwanda, na miji huko kusini mwa Lebanon na Bonde la Bekaa.
Israel imeendelea kufanya mfululizo wa mashambulizi ya anga katika maeneo yote ya kusini na mashariki mwa Lebanon, ikiendelea kukanyaga makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo lengo lake ni kukomesha uchokozi na uvamizi wa Tel Aviv dhidi ya uhuru na mamlaka ya kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu.