UN yatoa mwito wa kupunguzwa mvutano wa baada ya uchaguzi nchini Msumbiji
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka mvutano na machafuko ya baada ya uchaguzi nchini Msumbiji ambayo yameshapelekea watu 20 kupoteza maisha huku usalama ukizidi kudorora.
Volker Turk ametoa mwito huo kwenye taarifa maalumu akisema: "Nimekuwa nikifuatilia matukio ya Msumbiji ya baada ya uchaguzi kwa wasiwasi mkubwa, na nimesikitishwa sana na ghasia zilizoikumba nchi yote." Amesema: "Ghasia hazina nafasi katika michakato ya uchaguzi na, ni muhimu kuhakikisha kwamba malalamiko ya baada ya uchaguzi yanatatuliwa kwa amani kupitia mazungumzo jumuishi na michakato huru ya mahakama inayoendana na haki za binadamu na utawala wa sheria."
Kituo cha Demokrasia na Haki za Kibinadamu cha nchini Msumbiji kimesema kuwa hadi hivi sasa watu 24 wameshapoteza maisha kutokana na vurugu zilizojitokeza baada ya uchaguzi nchini humo. Ghasia zimeikumba nchi hiyo ya kusini mwa Afrika baada ya uchaguzi wa rais wa Oktoba 9 ambao Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza kuwa, Daniel Chapo wa chama tawala cha Mozambique Liberation Front (Frelimo) ameshindwa kwa asilimia 70 ya kura lakini wapinzani wamekataa kutambua matokeo hayo. Kiongozi wa upinzani, Venancio Mondlane, ambaye kwa mujibu uwa tume hiyo ameshika nafasi ya pili kwa asilimia 20.32 ya kura ameendelea kutoa mwito wa kupinga matokeo hayo akiyataja kuwa ni ya udanganyifu.
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, maandamano yaliyoanza Oktoba 21 yalichochewa na mauaji ya wawakilishi wawili wakuu wa kisiasa, Elvino Dias na Paulo Guambe. Taarifa ya ofisi hiyo pia imesema: "Polisi wanawarushia risasi waandamanaji na kusababisha vifo vya watu wengi na wanatumia kiholela mabomu ya kutoa machozi."