Kushadidi mgogoro wa Gaza kufuatia kusimamishwa shughuli za UNRWA
(last modified Thu, 07 Nov 2024 02:27:27 GMT )
Nov 07, 2024 02:27 UTC
  • Kushadidi mgogoro wa Gaza kufuatia kusimamishwa shughuli za UNRWA

Kutokana na tangazo la kusitishwa shughuli za UNRWA, taasisi za kimataifa zimeonya kuhusu uwezekano wa kuzorota zaidi hali ya maisha ya Wapalestina hususan watoto, wanawake na wagonjwa huko Ukanda wa Gaza.

Utawala wa Kizayuni umeutaarifu rasmi Umoja wa Mataifa kwamba umevunja uhusiano wake na UNRWA (shirika la misaada na ajira kwa wakimbizi wa Kipalestina katika Mashariki ya Karibu).

Knesset (bunge) ya utawala wa Kizayuni ilipitisha sheria dhidi ya UNRWA wiki iliyopita kwa kuidhinishwa na wawakilishi 92 dhidi ya upinzani wa wawakilishi 10, ambayo inapiga marufuku shughuli za UNRWA katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala huo pandikizi tangu mwaka 1948.

Tangazo rasmi la kusitishwa ushirikiano na UNRWA, ambalo limetangazwa wakati Gaza imekuwa chini ya vita na mashambulizi makali ya Wazayuni kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, limeongeza wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Wapalestina wanaoishi huko Gaza.

Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, (WHO) amesema katika muktadha huo: "Hakuna mbadala wa UNRWA. Kupigwa marufuku shughuli za UNRWA na Israel hakutaifa kuwa salama zaidi, bali kutaongeza mateso dhidi ya watu wa Gaza na kuongeza hatari ya kuzuka magonjwa."
Kwa mujibu wa ripoti zilizochapishwa, zaidi ya asilimia  70 ya miundombinu na nyumba za Wapalestina imeharibiwa tangu kuanza vita vya Gaza, na hatua ya sasa itafanya hali ya mambo huko Gaza kuwa mbaya zaidi.

Pia, wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na Joyce Mesoya, kaimu mratibu wa masuala ya dharura wa UNICEF, mkuu wa Mpango wa Chakula Duniani na mashirika ya misaada, wameonya vikali katika taarifa kwamba: "Wapalestina wote wanaoishi katika eneo la kaskazini mwa Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na hatari ya kifo kutokana na magonjwa, njaa kali na ghasia za kinyama."

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema, kupiga marufuku shughuli za (UNRWA) hakuufanyi utawala wa Kizayuni kuwa salama zaidi.

Hali ya mambo huko Gaza ni mbaya sana. Mashambulio ya mabomu ya utawala wa Kizayuni yanaendelea, miundombinu ya afya, vituo vya matibabu na hospitali zote zimeharibiwa, na upatikanaji wa dawa na madaktari umekuwa mgumu sana. Kwa upande mwingine, marufuku ya kusafiri inafanya iwe vigumu kuwafikishia misaada ya chakula na dawa Wapalestina waliosalia Gaza, ambapo wengi wao ni wanawake na watoto. Suala hilo limekuwa gumu zaidi sasa kufuatia kusimamishwa kabisa shughuli za UNRWA.

Catherine Russell, mkuu wa UNICEF, amesema katika taarifa yake ya hivi karibuni kuwa: "Mashambulizi ya  Israel yamedhihirisha sura nyingine mpya ya giza katika moja ya vipindi vya giza zaidi katika vita hivi vya kutisha."

Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa, katika kipindi cha siku tatu zilizopita, sio tu kwamba mashambulizi ya utawala wa Kizayuni yamepelekea kuuawa shahidi zaidi ya watoto 50 huko Jabalia, bali vikosi vya Israeli vimesimamisha kabisa shughuli za kliniki za chanjo ya polio kwa watoto kwa kurusha maguruneti kwenye kliniki na kujeruhiwa watoto na wafanyakazi wa UNICEF wanaofanya kazi kwenye kliniki hizo.

Philip Lazzarini, Kamishna wa UNRWA, ameonya kuhusiana na suala hilo kuwa: "Bila UNRWA, hatima ya mamilioni ya watu itakuwa hatarini na kutojulikana."

Kadhim Abu Khalaf, Msemaji wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) pia ameashiria hali mbaya ya watoto katika Ukanda wa Gaza na kusema: "Kinachoendelea huko Gaza kinakiuka wazi viwango vyote vya kimataifa na kukiuka vifungu vyote vya sheria za kimataifa."

Kwa hakika ukatili wa Israel katika mauaji ya raia na watoto wa Kipalestina katika vita vya Gaza ni mfano wa wazi wa mauaji ya kimbari yanayotekelezwa hadharani mbele ya macho ya walimwengu, ambapo nchi za Magharibi zinazodai kutetea haki za binadamu si tu zimeamua kukaa kimya bali zinashirikiana kikamilifu na utawala wa Kizayuni katika mauaji hayo ya kimbari kwa kuupa misaada ya kila aina ya kisiasa, kifedha na silaha.

Uungaji mkono wa nchi za Magharibi hususan Marekani kwa utawala huo pandikizi umepelekea juhudi za jamii ya kimataifa za kujaribu kusimamisha vita vya Gaza kutofanikiwa, ambapo sasa viongozi wa utawala huo wamepata kiburu zaidi na hata kuchukua hatua ya kupiga marufuku shughuli za UNRWA, ambao ni mlango pekee uliokuwa umebakia wazi kwa ajili ya kuwasaidia majeruhi na watoto wa Gaza.

Tags