Wanajeshi wa Nigeria waua magaidi 481 mwezi Oktoba
Jeshi la Nigeria limetoa taarifa na kusema kuwa, takriban magaidi 481 wameuawa na wengine zaidi ya 741 wametiwa mbaroni na wanajeshi wa nchi hiyo katika operesheni za kupambana na ugaidi zilizofanyika kwenye kona zote za Nigeria katika mwezi uliopita wa Oktoba.
Msemaji wa jeshi hilo, Edward Buba amewaambia waandishi wa habari katika taarifa yake ya kila mwezi mjini Abuja kwamba, mbali na kuuawa na kujeruhiwa idadi hiyo kubwa ya magaidi, jeshi la Nigeria limefanikiwa pia kukomboa zaidi ya mateka 492 kutoka mikononi mwa watekaji nyara hao katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, katika muda huo, jumla ya silaha 480 na risasi 9,026 za aina mbalimbali zimepatikana zikiwa mikononi mwa magaidi hao.
Aidha Buba amebainisha kuwa, wanajeshi wa Nigeria wamesambaratisha kwa kiasi kikubwa maficho ya magenge ya wahalifu katika kona mbalimbali za nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Magaidi walikuwa wanatumia maficho hayo kufanyia mazoezi, kuficha silaha zao na kupanga vitendo vya kigaidi na kihalifu.
Ameongeza kuwa, mkakati wa jeshi la Nigeria ni kudhoofisha kikamilifu uwezo wa magenge ya wahalifu popote yalipo nchini humo.