Sababu zilizopelekea Trump kushinda uchaguzi wa rais wa Marekani
(last modified Fri, 08 Nov 2024 06:59:39 GMT )
Nov 08, 2024 06:59 UTC
  • Sababu zilizopelekea Trump kushinda uchaguzi wa rais wa Marekani

Hatimaye mchuano mkali uliowaweka watu roho juu, wa kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais wa Marekani wa 2024 uliofanyika Novemba 5, umemalizika na matokeo yake rasmi yametangazwa.

Baada ya kukamilika zoezi la kuhesabu kura za uwakilishi katika majimbo (electoral college), mgombea wa chama cha Republican Donald Trump ameibuka mshindi rasmi wa uchaguzi huo kwa kunyakua kura 295. Mgombea wa chama cha Democratic Kamala Harris alipata kura 226 za uwakilishi huo wa majimbo.

Kushindwa Harris katika uchaguzi huo wa rais na Trump kwa ushindi wa kishindo ni jambo ambalo halikutarajiwa. Harris alikuwa akionekana kila mara amemwacha nyuma Trump katika chunguzi kadhaa za maoni zilizofanywa katika miezi ya karibuni na vyombo vya habari na vituo vya uchunguzi wa maoni. Suala hili lilihusisha pia majimbo saba yasiyotabirika. Hata hivyo, siku chache tu kabla ya uchaguzi, hali ilibadilika katika majimbo hayo yanayojulikana pia kama majimbo ya mpambano, kwa Trump kumpita Harris katika mengi kati yao au kumkaribia sana kwa kura.

Biden na Harris

Suala linalovisumbua sana vichwa vya wataalamu wa mambo sasa hivi kuliko wakati mwingine wowote ni kutaka kujua ni sababu gani zilipelekea Trump kupata ushindi katika uchaguzi wa rais wa 2024? Huenda sababu zote hizo zikaweza kukusanywa ndani ya kapu la sababu moja kuu, kwa kuichanganua sababu hiyo katika pande tofauti. Sababu hiyo moja kuu ni manung'uniko makubwa ya Wamarekani ya kutoridhishwa na hali ya sasa hivi ya nchi yao, na kuwa na matumaini kwamba labda hali itabadilika kwa kuingia madarakani rais mpya, ambaye aliwahi hapo kabla kuwepo kwenye Ikulu ya White House.

Seneta wa chama cha Republican Lindsey Graham ameandika yafuatayo kwenye mtandao wa kijamii wa X kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais wa Marekani: "matokeo haya yasitafsiriwe kuwa ni kitendawili, wakati 70% ya wananchi wanaamini kwamba, Marekani inafuata mkondo usio sahihi; na wakati mgombea wa Wademokrati ambaye ndiye makamu wa rais anaielekeza Marekani kwenye njia isiyo sahihi, kwa hiyo uwezekano mkubwa ni kuwa nyinyi mtashindwa. Kwa lugha nyepesi ni kuwa, miaka minne iliyopita imewaletea masaibu mengi Wamarekani, kiasi kwamba hawawezi kujimudu kimaisha kutokana na kupanda kwa bei za vitu na mishahara isiyoongezwa. Dunia inatokota moto kwa maana halisi ya hilo neno. Kutarajia ushindi (kwa Wademokrasia) katika hali hii halikuwa jambo linalokubalika kamwe".

Ukweli ni kwamba, kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa rais wa 2020, ambapo Wamarekani walimpigia kura mgombea wa chama cha Democratic Joe Biden wakiwa na matumaini ya hali kuboreka baada ya kukatishwa tamaa na utendaji wa Trump na tabia yake ya ajabu ajabu, pamoja na kashfa kadhaa zilizomwandama; sasa hivi pia, baada ya miaka minne ya hali ngumu, hususan kutokana na mfumuko mkubwa wa bei ambao haujawahi kushuhudiwa katika miaka thelathini ya karibuni, kuongezeka kwa bei ya mafuta, kuzidi hali kuwa mbaya katika kadhia ya wahamiaji haramu, pamoja na kutoridhishwa na sera na muelekeo wa serikali ya Biden kuhusiana na vita vya Ukraine na vita katika Ghaza, yote hayo inaonekana yameifanya zaidi ya 50% ya Wamarekani kufikia hitimisho kwamba, wana kila sababu ya kumuamini na kumpigia kura Trump kwa ahadi alizotoa, hususan katika suala la kuboresha hali ya uchumi na kukabiliana vikali na wahamiaji haramu.

Katika matokeo ya karibuni zaidi ya uchunguzi wa maoni uliofanywa kabla ya uchaguzi ilibainika kuwa Wamarekani wanamwamini Trump katika suala la uchumi na kushughulikia tatizo la wahajiri haramu, na wana imani na Harris katika kulinda demokrasia na kudhamini bima ya afya kwa wote.

Hapana shaka kuwa, rekodi ya Biden katika sera za nje, ambayo anahusika nayo pia Kamala Harris akiwa ni makamu wake wa rais, haikubaliki. Katika miaka ya karibuni, utawala wa Biden umetoa makumi ya mabilioni ya dola kuisaidia kijeshi na kwa silaha Ukraine, katika vita na mmoja wa maadui wakuu wa Marekani, yaani Russia, suala ambalo limepingwa vikali na Warepublican, akiwemo Trump.

Aidha, tangu vilipoanza vita vya Ghaza, badala ya kufanya juhudi za kuvikomesha, serikali ya Biden ilitoa msaada wa silaha wa karibu dola bilioni 19 kwa Israel na hivyo kubeba dhima ya kuhusika moja kwa moja katika kuendeleza vita hivyo na mauaji ya kimbari ya Wapalestina yanayofanywa na Utawala wa Kizayuni.

Wapinzani wa vita vya Ghaza ndani ya Bunge la Marekani

Hatua hiyo ya Biden ilikabiliwa na upinzani mkubwa ndani ya Marekani wa vijana na hasa wanachuo na kupelekea kuibuka vuguvugu la wanachuo wanaowaunga mkono Wapalestina kukabiliana na sera hiyo ya serikali ya Biden. Naye Kamala Harris, akiwa makamu wa rais wa Biden, badala ya kufanya juhudi athirifu na za adhati za kuhitimisha vita vya Ghaza kwa kuanzia na usimamishaji mapigano, alitosheka na kutoa kauli tu zisizo na taathira yoyote katika suala hilo; na badala yake akatoa sisitizo mara kadhaa la kuiunga mkono Israel wa kila hali.

Sababu zote hizi tulizoashiria, za ndani na nje, ziliifanya sehemu kubwa ya jamii ya Marekani ipoteze matumani kwa chama cha Democrat na mgombea wake Kamala Harris na hivyo kumgeukia Donald Trump, mgombea wa Republican katika uchaguzi wa rais wa 2024, kwa matumaini kwamba huenda ataboresha mazingira na hali ya ndani na nje ya Marekani.../

 

Tags