Takriban watu 11 wameuawa katika shambulio la RSF katikati mwa Sudan
Takriban watu 11 wameuawa na wengine 18 kujeruhiwa katika shambulio lililofanywa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika kijiji cha al Hodur cha Jimbo la Gezira, katikati mwa Sudan.
Shirika la Madaktari wa Sudan ambalo si la kiserikali limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, washambuliaji wa kundi la RSF wamefanya uporaji pia katika kituo cha afya cha kijiji hicho na kwenye nyumba za raia na kwamba miongoni mwa waliouawa ni wanawake na watoto wadogo.
Wakati huo huo "Jukwaa la Nidaa Al-Wasat" ambalo ni kundi la kujitolea linalofuatilia ukiukwaji wa haki za binadamu limeripoti kwamba idadi ya watu waliouawa katika mji wa al Hilaliya wa Jimbo la Gezira na ambao walikuwa wamezingirwa kwa zaidi ya siku 17 na kundi la RSF, imeshpindukia watu 300.
Hadi wakati tunaripoti habari hii kundi la RSF lilikuwa bado halijatoa maelezo yoyote kuhusu mauaji ya mji wa Al Hilaliya.
Wanaharakati wa ndani na makundi ya kujitolea yanalishutumu kundi la RSF kwa kuanzisha mashambulizi mashariki mwa Jimbo la Gezira baada ya kamanda wake wa ukanda huo, Abu Aqla Keikel kujisalimisha kwa Jeshi la Sudan (SAF) tarehe 20 Oktoba 2024.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu iliripoti Jumanne kwamba karibu watu 135,400 wameyakimbia makazi yao katika Jimbo la Gezira tangu Oktoba 20 kutokana na kuongezeka mashambulizi katika vijiji na miji zaidi ya 30 ya jimb hilo.