Hizbullah yaendelea kutoa vipigo, sasa imepiga wizara ya vita ya Israel
(last modified Thu, 14 Nov 2024 02:44:07 GMT )
Nov 14, 2024 02:44 UTC
  • Hizbullah yaendelea kutoa vipigo, sasa imepiga wizara ya vita ya Israel

Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon jana Jumatano uliitwanga kwa mara ya kwanza wizara ya vita ya utawala wa Kizayuni mjini Tel Aviv kwa kutumia ndege zisizo na rubani, likiwa ni shambulio la aina yake na la mara ya kwanza tangu vilipoanza vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Muqawama wa Lebanon na Palestina.

Hizbullah imetoa taarifa rasmi na kusema kuwa ikiwa ni kuendelea na operesheni zake za kishujaa za kujibu jinai za Israel huko Palestina na Lebanon, Muqawama wa Lebanon umeshambulia kituo kikuu kinachoendesha vita vya kijinai cha Israel ambapo ndipo ilipo komandi kuu ya jeshi la utawala wa Kizayuni. 

Kabla ya hapo pia, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah, ilikuwa imetangaza kwamba, kwa mara ya kwanza, imeshambulia kwa makombora kambi kubwa ya jeshi la anga la utawala wa Kizayuni wa Israel, ikiwa ni sehemu ya ulipizaji kisasi dhidi ya ukatili unaofanywa na utawala huo ghasibu.

Hizbullah ya Lebanon yaendelea kutoa vipigo vikali kwa utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Hizbullah imetangaza kuwa imeilenga kambi ya HaHotrim, ambayo ni kituo muhimu sana cha makazi ya askari wa jeshi la anga la utawala wa Kizayuni, kinachojumuisha miundo ya usafirishaji na kiwanda cha injini.

Kituo hicho kiko kusini mwa mji unaokaliwa kwa mabavu wa Haifa, yapata kilomita 40 kutoka mpaka wa Lebanon na Palestina.

Taarifa ya Hizbullah imesema, shambulio hilo ni sehemu ya mfululizo wa operesheni za Khaybar, ambazo zinavilenga vituo nyeti vya kijasusi vya utawala wa Kizayuni na maeneo yake mengine ya kimkakati.

Mbali na operesheni hiyo, Hizbullah imeshambulia pia kwa msururu wa ndege zisizo na rubani kituo cha kamandi ya Brigedi ya Ramim kwenye kambi ya Hunin na kuzilenga kwa usahihi shabaha zilizokusudiwa.