Netanyahu ni mhalifu wa kivita, atakamatwa akikanyaga Dearborn Marekani
Mji mmoja nchini Marekani umeahidi kumkamata Waziri Mkuu wa utawala wa Israel, Benjamin Netanyahu, na waziri wake wa zamani wa vita, Yoav Gallant, iwapo watakanyaga kwenye mji huo baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC, kutoa vibali vya kuwakamata kutokana na jinai zao za kivita na na mauaji ya kimbari yanayoendelea Ukanda wa Gaza.
Abdullah Hammoud, meya wa Dearborn katika jimbo la Michigan, amesema kwamba viongozi wa eneo hilo "watamkamata Netanyahu na Gallant ikiwa wataingia ndani ya mipaka ya jiji la Dearborn," akitoa wito kwa miji mingine ya Marekani kuiga mfano huo.
Katika chapisho lake kwenye mtandao wa X ameandika: "Miji mingine inapaswa kutangaza vivyo hivyo. Rais wetu anaweza asichukue hatua, lakini viongozi wa jiji wanaweza kuhakikisha Netanyahu na wahalifu wengine wa kivita hawakaribishwi kusafiri kwa uhuru kote Marekani."
Matamshi hayo yalikuja baada ya mahakama ya ICC, yenye makao yake makuu mjini The Hague, kuamua kuwa kuna "sababu za kuridhisha" za kuamini kuwa Netanyahu na Gallant wanabeba dhima kama washiriki wa "uhalifu wa kivita wa kutumia njaa kama mbinu ya vita; na uhalifu dhidi ya ubinadamu wa mauaji, mateso, na vitendo vingine visivyo vya kibinadamu”.
Katika taarifa yake, jopo la majaji watatu wa ICC, limesema limekataa pingamizi la Israel dhidi ya mamlaka ya mahakama hiyo na kutoa vibali dhidi maafisa wa utawala huo.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amesema vibali vya ICC vya kutaka kukamatwa waziri mkuu wa Israel na waziri wake wa zamani wa vita si vya kisiasa na kwamba nchi zote wanachama wa EU zinapaswa kuheshimu uamuzi wa mahakama na kuutekeleza.
Nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Uholanzi, Uswizi, Ireland, Kanada, Italia na Uhispania, zimetangaza bayana kwamba zitatimiza majukumu yao kuhusu Mkataba wa Roma na sheria za kimataifa, zikimaanisha kuwa ziko tayari kumkamata Netanyahu na waziri wake wa zamani wa vita iwapo watafika katika nchi hizo..
Israel ilianzisha mashambulizi yake ya mauaji ya kimbari kwenye Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba 2023, baada ya kundi la muqawama la Hamas kutekeleza oparesheni yake ya kihistoria dhidi ya utawala huo ghasibu kwa lengo la kulipiza kisasi jinai zinazozidi kufanywa na utawala huo dhidi ya watu wa Palestina.
Utawala wa haramu wa Israel hadi sasa umewaua Wapalestina wasiopungua 44,056, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi wengine 104,268, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza.