Uganda yatangaza kumalizika kwa mlipuko wa homa ya Ebola nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140252-uganda_yatangaza_kumalizika_kwa_mlipuko_wa_homa_ya_ebola_nchini_humo
Mamlaka nchini Uganda zimetangaza kuwa nchi hiyo sasa haina maambukizi ya virusi vya Ebola, huku maambukizi ya ugonjwa huo wa homa ya kutokwa damu yakiendelea kuongezeka katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
(last modified 2026-07-29T14:18:41+00:00 )
Jul 29, 2026 14:16 UTC
  • Waziri wa Afya wa Uganda, Chris Baryomunsi
    Waziri wa Afya wa Uganda, Chris Baryomunsi

Mamlaka nchini Uganda zimetangaza kuwa nchi hiyo sasa haina maambukizi ya virusi vya Ebola, huku maambukizi ya ugonjwa huo wa homa ya kutokwa damu yakiendelea kuongezeka katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Waziri wa Afya wa Uganda, Chris Baryomunsi, mnamo Jumanne alitangaza “kukamilika kwa mafanikio kwa kipindi cha lazima cha uangalizi cha siku 42 kilichoanza baada ya kuruhusiwa kwende nyumbani kwa raia wa mwisho wa Uganda, aliyekuwa mgonjwa aliyeambukizwa ndani ya nchi, mnamo Juni 16, 2026.”

Baryomunsi amesema: “Katika kipindi chote hiki, Wizara ya Afya iliendeleza uangalizi mkali nchi nzima, na hakuna kesi mpya za Ebola zilizogunduliwa.”

Katika taarifa ya baadaye kupitia mitandao ya kijamii, Baryomunsi aliwasihi Waganda “kuendelea kuwa macho” na kuendelea kuzingatia hatua za afya ya jamii.

Kati ya wagonjwa 20 waliothibitishwa, 18 waliruhusiwa kurejea nyumbani huku wawili wakifariki dunia kutokana na ugonjwa huo. Wote waliofariki walikuwa wakitokea DRC, ambako mlipuko mkubwa zaidi umekuwa ukiendelea tangu katikati ya mwezi Mei.

Wakati huo huo, kulingana na takwimu za Jumanne kutoka Wizara ya Afya ya DRC, kumekuwa na angalau maambukizi 3,262 nchini humo, huku watu 1,437 wakipoteza maisha. Hali hii inakaribia kufanana na mlipuko wa mwaka 2018-2020 ambao ndio mkubwa zaidi kuwahi kurekodiwa nchini humo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa mlipuko wa hivi karibuni wa Ebola nchini DRC ndio unaosambaa kwa kasi zaidi kuwahi kurekodiwa, na kwamba ukubwa wake halisi unaweza kuwa mara mbili hadi nne zaidi ya takwimu zinazoripotiwa.

Aina ya virusi vinavyosambaa nchini DRC ni Bundibugyo, ambayo ni nadra zaidi kati ya aina nne za Ebola zinazojulikana kuathiri binadamu, na kwa sasa haina chanjo wala matibabu yaliyoidhinishwa.

Ebola ni ugonjwa wa virusi wa homa ya kutokwa damu ambao unaweza kusababisha homa kali, kutapika, kuhara, na kutokwa damu kwa ndani. Husambaa kupitia mgusano wa moja kwa moja na majimaji ya mwili ya watu wanaoumwa na virusi hivyo au wale waliokwisha kufariki kutokana na ugonjwa huo.