Tanzania: Watu watano wafariki dunia baada ya jengo kuporomoka Kariakoo
Watu watano wamefariki dunia, na zaidi ya 40 kujeruhiwa baada ya jengo kuporomoka katika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, nchini Tanzania.
Hayo yameelezwa Jumamosi na Mrakibu Msaidizi wa Polisi Peter Mtui ambaye anasimamia zoezi la uokoaji katika jengo hilo.
Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi amesema wamepokea majeruhi 42 mpaka sasa.
Shughuli ya uokoaji inaendelea huku wananchi wakishirikiana na vyombo vya dola ikiwemo jeshi la Zimamoto.
Kuna hofu huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kassim amefika katika eneo hilo na kuzungumza na wanahabari akisema zoezi la uokoaji linaendelea ili kuhakikisha waliofunikwa na kifusi wanatoka wakiwa hai.
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa walioathirika na mkasa huo.
Kwa mujibu wa mashuhuda ghorofa hilo lilianguka ghafla majira ya saa tatu asubuhi wakati mafundi wa ujenzi walipokuwa wakiendelea na shughuli ya kuongeza maduka.
Maelfu ya raia katika soko hilo wamesimamisha shughuli zao wakisubiri kuwaona ndugu zao waliofukiwa na kifusi katika jengo la ghorofa tano lililoporomoka saa tatu asubuhi leo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamia amesema, majeruhi wamepelekwa Hospitali ya taifa ya Muhimbili.
Kwa mujibu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji walipokea taarifa ya kuanguka kwa Jengo Kariakoo, vikosi vya kamandi zote za Mkoa Dar es Salaam viko katika tukio hilo na kuendelea na uokoaji.
“Zoezi la uokoaji linaendelea tayari tumefanikiwa kuokoa watu sita wakiwa hai” Tunawasihi wananchi kutulia kwani tupo imara na tunaendelea na jitihada za uokoaji kwa kushirikiana na vyombo vingine,'' aliongeza Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Naibu Kamishna Puyo Nzalayaimisi.