Wananchi wa Gabon washiriki kura ya maoni ya marekebisho ya katiba
Raia wa Gabon wamepiga kura ya maoni ya kuidhinisha katiba mpya katika hatua ambayo inaonekana kuwa muhimu kwa ajili ya kurejesha utawala wa kiraia katika taifa hilo la Afrika ya Kati.
Upigaji kura ulianza mwendo wa saa moja asubuhi kwa saa za Gabon katika vituo 2800 vya kupigia kura ili kupigia kura ya ndiyo au hapana rasimu ya katiba mpya.
Kura hiyo ya maoni inaonekana kuwa hatua muhimu zaidi katika mchakato ulioanzishwa baada ya mapinduzi ya kijeshi mwezi Agosti 2023.
Rais wa mpito Brice Oligui Nguema alichukua mamlaka katika mapinduzi ya mwaka jana, na kumuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Ali Bongo ambaye alikuwa ameshinda uchaguzi wa marudio.
Uchaguzi umepangwa kufanyika Agosti 2025, na Jenerali Nguema anaweza kugombea, kulingana na baadhi ya wachambuzi wa kisiasa. Katiba mpya ikipitishwa itampa mamlaka ya kushindana.
Wanaounga mkono katiba inayopendekezwa wanasema, rasimu ya hiyo ya sheria inawakilisha kujiondoa kwenye utawala wa miaka 55 wa familia ya Bongo.
Lakini wakosoaji wanasema inaweza kumpatia rais madaraka makubwa zaidi, na wanahofia hatua hiyo inaweza kumuingiza madarakani mtawala mpya.