Jenerali wa Nigeria: Magaidi, waasi barani Afrika wanatumia silaha za Israel
Jenerali mstaafu wa jeshi la Nigeria ambaye alikwenda katika nchi kadhaa za Afrika zikiwemo Mali na Liberia kwa ajili ya kulinda amani, amefichua kuwa silaha nyingi walizozikamata kutoka kwa magaidi na waasi wa nchi tofauti zinatoka Israel, jambo ambalo limeweka wazi mkono wa Wazayuni katika migogoro na ugaidi unaotokea katika baadhi ya nchi za Afrika.
Katika mahojiano maalumu na Iran Press mjini Abuja, kuhusiana na hali ya sasa ya Mashariki ya Kati, Jenerali Garus Gololo amempongeza Rais Bola Ahmad Tinubu ambaye ametoa wito wa jamii ya kimataifa kuchukua hatua kali za kukomesha mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Palestina kwa kuitangaza Palestina huru, mji mkuu wake ukiwa Quds tukufu.
Gololo ameongeza kuwa: "Waisraeli walikwenda Palestina kama wageni lakini baadaye waliteka karibu ardhi yote ya nchi hiyo. Wanaendelea kuua watu. Mimi ni afisa mstaafu wa jeshi, na linapokuja suala la vita, hushambulii hospitali, misikitini, shule, wala huui watoto. Lakini Israel inafanya haya yote, na wanaua hata wanawake wenye mimba.”
Jenerali huyo mstaafu wa Nigeria ameeleza kuwa: "Ninavyofahamu mimi, haya ni mauaji ya kimbari. Hii haijawahi kutokea duniani."
Jenerali Gololo ambaye ni chifu wa chama tawala cha Nigeria, APC, amehoji unafiki wa Marekani na washirika wake wa Magharibi ambao wamekuwa wakitetea misimamo yao kuhusu mzozo wa Russia na Ukraine na kufumbia macho mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel. Ameuliza: “Kwa nini Marekani na washirika wake wanaizungumzia Ukraine lakini wameifumbia macho Gaza? Kuna tofauti gani kati ya damu ya watu wa Ukraine na ile ya Wapalestina? Hivi wote ni wanadamu?"
Ameongeza kwa kusema: "Wanaipa Ukraine silaha za kupigana na Russia lakini kwa nini pia hawawapi Wapalestina silaha ili kujilinda katika mauaji ya Israel? Wanawaita Wapalestina magaidi, lakini Netanyahu ndiye gaidi mkubwa zaidi."