Msumbiji: Upinzani watoa wito kuomboleza vifo vya watu 50
(last modified Thu, 21 Nov 2024 03:45:23 GMT )
Nov 21, 2024 03:45 UTC
  • Msumbiji: Upinzani watoa wito kuomboleza vifo vya watu 50

Kiongozi wa upinzani nchini Msumbiji Venancio Mondlane ametoa wito wa kufanyika siku tatu za maombolezo kuanzia jana Jumatano kutokana na vifo vya watu 50 aliosema waliuawa katika ghasia za baada ya uchaguzi wa Oktoba 9.

Katika chapisho kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Mondlane ametaka pia kuhesabiwa upya kura baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza Daniel Chapo wa chama cha Frelimo kilichopo madarakani kwa karibu nusu karne kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi anayetakiwa kuondoka madarakani mwezi Januari alilihutubia taifa siku ya Jumanne na kulaani "jaribio la kuanzisha machafuko katika nchi hiyo" huku akihimiza kufanyike mazungumzo ili kumaliza machafuko yaliyodumu kwa wiki kadhaa.

Watu wasiopungua 30 wanaripotiwa kuuawa katika maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi kufuatia ushindi wa mgombea wa chama tawala cha FRELIMO Daniel Chapo. Ghasia hizo ziliikumba katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika baada ya uchaguzi wa rais wa Oktoba 9, ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza kuwa, Daniel Chapo wa chama tawala cha Mozambique Liberation Front (Frelimo) ameshinda kwa asilimia 70 ya kura, lakini wapinzani wamekataa kutambua matokeo hayo.