Rais Ruto: Maandamano ya mwezi Juni yalijaa uhuni
Rais William Ruto wa Kenya ameonekana kutetea mienendo ya maafisa wa polisi waliodaiwa kuhangaisha waandamanaji mwezi Juni 2024, wakati wa maandamano dhidi ya serikali yake.
Akilihutubia taifa leo Alkhamisi, Novemba 21, 2024, Rais Ruto amesema licha ya serikali yake kuheshimu haki za Wakenya kuandamana, lakini maandamano yaliyoshuhudiwa mwaka huu yalijaa uhuni.
“Tunaheshimu demokrasia na uhuru wa kujielezea, ila maandamano yaliyoshuhudiwa ilikuwa vigumu kutambua waandamanaji halali na wahalifu. Yalisheheni uhuni,” amesema Rais William Ruto akihutubu Bunge.
Ameongeza kuwa maafisa usalama walikabiliwa na wakati mgumu kulinda maisha ya watu, mali na biashara zao.
Amesisitiza kuwa: “Serikali itaendelea kulinda maisha ya watu na mali dhidi ya wahuni.”
Mwezi Juni mwaka huu, vijana wa Gen Z walishiriki maandamano ya kitaifa kukosoa serikali, hasa Muswada tata wa Fedha 2024 uliokuwa umepitishwa na Bunge.
Rais William Ruto alilazimika kufutilia mbali muswada huo kutokana na maandamano na machafuko makubwa yaliyoikumba Kenya.
Maandamano hayo yalisababisha mvifo vya vijana zaidi ya 60, huku mashirika ya kutetea haki za kibinadamu na wanaharakati wakinyooshea kidole cha lawama serikali ya Kenya Kwanza kwa kuendeleza utawala wa kiimla na utekaji nyara wa waandamanaji.
Hotuba ya leo ya Rais Ruto inakuja wakati serikali yake ikiendelea kulaumiwa kutokana na visa utekaji nyara wa watu, ufisadi na sera za kiuchumi ambazo zinakosolewa na wapinzani wake.