Mapigano mapya yazuka katika mji mkuu wa Sudan Kusini
Mapigano makali ya bunduki yamezuka, katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, baada ya vikosi vya usalama kwenda kumkamata mkuu wa idara ya ujasusi.
Mapigano hayo ambayo kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, yalizuka jana Alkhamisi jioni yameibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa raia.
Ripoti zinasema kuwa, mapigano yalianza majira ya saa moja usiku kwa saa za huko, na kuendelea mfululizo kwa saa moja kabla ya kumalizika amesema ripota wa Reuters.
Tahadhari kwenda kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa ambayo Reuters iliona, ilieleza kwamba mashambulizi yalihusiana na kukamatwa kwa mkuu wa zamani wa idara ya taifa ya ujasusi ama NSS. Umoja wa Mataifa umewataka wafanyakazi wake kujificha maeneo salama.
Mapema Oktoba, rais Salva Kiir, alimfuta kazi Akol Koor Kuc, ambayo aliongoza NSS toka nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka Sudan, 2011, na alimteua mshirika wake wa karibu kuongoza idara ya ujasusi.
Nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ilitumbukia kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu makamu wake wakati huo, Machar kuwa alipanga njama ya kumpindua.