Mwisho wa domino ya kuwafukuza wanajeshi wa Ufaransa kutoka Afrika ya Kati
Msemaji wa jeshi la Chad ametangaza kwamba nchi hiyo ilipokea kambi ya mwisho ya jeshi la Ufaransa Alhamisi, Januari 30.
Mnamo Novemba 2024, Chad ilitangaza kumalizika muda wa makubaliano ya ushirikiano wa kiusalama na kiulinzi na Ufaransa, na vikosi vya jeshi la Ufaransa vilianza kuondoka Chad Desemba 10.
Rais wa Chad, Mahamat Idriss Déby Itno alitangaza Desemba 31, 2024, kwamba kuondoka kwa vikosi vya Ufaransa nchini humo kutakamilika Januari 31. Jeshi la Ufaransa lilikuwa na wanajeshi wapatao 1,000 nchini Chad. Waziri wa Ulinzi wa Chad, Issakha Maloua Djamous, hapo awali alisema kwamba tarehe ya mwisho ya kuondoka wanajeshi wa Ufaransa nhini humo, Januari 31, "haiwezi kutenguliwa," na "haiwezi kujadiliwa."
Kuondolewa wanajeshi wa Ufaransa nchini Chad, baada ya kufukuzwa wanajeshi wa nchi hiyo huko Mali, Burkina Faso na Niger, kunahitimisha miongo kadhaa ya uwepo wa jeshi la Ufaransa katika eneo la Sahel barani Afrika. Majeshi ya Ufaransa yaliendelea kuwepo huko Chad baada ya nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1960 na katika nchi nyingine makoloni yake barani Afrika kwa kutumia visingizio mbalimbali. Kwa hakika, uhuru wa nchi za Kiafrika chini ya tawala za kikoloni za nchi za Ulaya, hasa Ufaransa, haukukomesha kukoloniwa nchi za bara hilo. Tangu wakati huo Afrika ilikabiliana na aina mpya ya ukoloni, unaojulikana kama ukoloni mamboleo. Kufukuzwa wanajeshi wa Ufaransa katika nchi za Kiafrika kunaashiria mwanzo wa mwisho wa ukoloni mamboleo na mwanzo wa zama mpya kwa nchi za Kiafrika. Kuhusiaina na suala hilo, Taasisi ya Sera ya Kimataifa ya Austria imesema katika uchambuzi wake kwamba, hatua ya nchi za Afrika ya Kati na Magharibi ya kuwafukuza wanajeshi wa Ufaransa ni sehemu ya mchakato mpana zaidi wa kupigania uhuru na msisitizo wa kujitawala, ambao unaweza kutajwa kuwa ni wimbi la pili la kung'oa ukoloni barani Afrika.
Uchambuzi wa taasisi hiyo ya wanafikra ya Austria unaendelea kusema: Mnamo tarehe 28 Novemba mwaka jana, saa chache tu baada ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrow huko N'Djamena, serikali ya Chad ilitangaza rasmi kumalizika kwa muda wa makubaliano ya ulinzi ya 1976 na Ufaransa. Siku hiyo hiyo, Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, pia alitangaza kwamba Ufaransa itafunga kambi zake za kijeshi nchini humo kwa sababu kuwepo kwa jeshi la nchi hiyo nchini humo ni kinyume na uhuru na mamlakka ya kujitawala ya taifa la Senegal.
Tovuti ya Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Umoja wa Ulaya inasema kwamba matukio haya ni vipande vya mwisho vya domino za mchezo wa kuporomoka ambao, kwa mujibu wa Dagauh Komenan, mwanahistoria na mtaalamu wa masuala ya Afrika, ulianza mwaka 2017.
Kwa upande wake, Djenabou Cisse, mtafiti katika Taasisi ya Utafiti wa Kimkakati yenye makao yake Paris, amedokeza kuwa kwa upande wa Ufaransa kuna hisia kwamba uwepo wa kijeshi barani Afrika ni moja ya alama za mwisho za nguvu ngumu (hard power) na utambulisho wa Ufaransa kama nguvu kubwa ya kimataifa, na sasa alama hiyo inafifia na kuyoyoma.
Anasema Ufaransa iliweza kuimarisha ushawishi wake barani Afrika kupitia mapinduzi 30 ya kijeshi kati ya 1964 na 2012; Ushawishi ambao umekuwa ukipungua kadiri muda unavyopita.
Mwishoni mwa miaka ya 1990, kuliibuka kizazi kipya katika bara zima la Afrika, kilichopigania uhuru na kujitawala, na sasa kinadhihirika katika harakati za kisiasa na kijamii. Jambo hili ni mojawapo na majibu ya swali kwamba, kwa nini hatua hizi zimechukuliwa kwa wakati huu? Na ni mambo gani yamechangia katika matukio haya, miaka 65 baada ya uhuru wa makoloni ya Ufaransa katika Afrika Magharibi na Kati? Naam, ni kuibuka kizazi cha vijana wanaharakati na chenye maarifa na uelewa kinachotaka mabadiliko ya kweli kupitia mawasiliano na mitandao ya kijamii.
Sababu nyingine inayochochea mwelekeo mpya wa matukio barani Afrika ni kuibuka kwa mfumo wa ulimwengu wa kambi kadhaa, ambao kielelezo chake kinaonekana katika kuongezeka nafasi wachezaji wengine wa kimataifa kama vile Uchina na Urusi katika bara la Afrika. Washirika hawa wapya ambao hawana historia ya ukoloni barani Afrika, wanatoa fursa za ushirikiano katika ngazi za kiuchumi na kijeshi bila kuingilia masuala ya ndani ya nchi za Afrika.