Kwa nini nchi za Kiafrika zinawafukuza wanajeshi wa Ufaransa?
Domino ya kuwafukuza wanajeshi wa Ufaransa katika nchi za Kiafrika inaendelea, na katika wiki zijazo, vikosi vya jeshi la Ufaransa pia vitaondoka Ivory Coast.
Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast hivi karibuni alitangaza kuondoka wanajeshi wa Ufaransa nchini humo katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2025 na kusema: "Tunaweza kujivunia jeshi letu, ambalo sasa ni la kisasa; na ni katika muktadha huu ndio tumeamua kuhusu kuondoka kwa mpangilio nchini kwetu wanajeshi wa Ufaransa." Tarehe ya kuondoka wanajeshi wa Ufaransa Ivory Coast imeshaainishwa yaani kuanzia tarehe 20 mwezi huu wa Februari.
Mkakati wa kuwafukuza wanajeshi wa Ufaransa katika nchi za Kiafrika ulianza kutekelezwa katika miaka michache iliyopita, huku Ufaransa ikiwa inadhibiti moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja akthari ya nchi za Kiafrika hasa zile za eneo la Sahel na za magharibi mwa bara hilo. Ni wazi kuwa Paris haijatumia tu utajiri wa maliasili na nafasi ya kistratijia ya nchi nyingi za Kiafrika, bali imepanua udhibiti wake katika nchi mbalimbali za bara hilo na kujiimarisha kijeshi kwa kisingizio cha kudumisha amani, usalama na kupambana na makundi ya kigaidi.
Licha ya siasa zote hizo za Ufaransa, lakini katika miaka ya karibuni na kufuatia kuongezeka mwamko wa kisiasa na mabadiliko ya msingi katika jamii tofauti za Kiafrika, nchi nyingi za bara hilo zinapigania uadilifu na wala hazikubali tena uwepo wa nchi za kigeni na kikoloni kama Ufaransa katika ardhi zao. Nyingi ya nchi hizo ambazo zimepitia mateso na machungu ya ukoloni, hivi sasa zimechukua mkondo wa ustawi na maendeleo ya kisiasa na kiuchumi na zinataka kutumia upeo wa juu wa fursa zilizopo katika nyanja hizo, kwa hiyo hazikubali tena uwepo wa wageni na sera zao za kikoloni.
Kuanza kutimuliwa wanajeshi wa Ufaransa katika nchi tofauti za Kiafrika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, ukosolewaji wa siasa za Ufaransa barani Afrika, kuundwa jumuiya za ushirikiano wa kieneo na kupanuliwa uhusiano wa kibiashara, kiuchumi na kisiasa katika ngazi za kieneo na kimataifa ni miongoni mwa ishara zinazoonyesha kuwa nchi za Afrika hazikubali tena siasa za ukoloni wa Ufaransa. Kuhusiana na hili, Rais Mahamat Idriss Deby wa Chad, amesema: 'Viongozi wa Ufaransa wanapasa kuwaheshimu watu wa Afrika.'
Katika mwaka mmoja uliopita, nchi hizi zimekuwa zikitekeleza siasa zao kwa namna ambayo viongozi wa Ufaransa wamelazimika kukubali mabadiliko ya kimsingi yanayotokea katika medani ya kisiasa na kijamii barani Afrika. Kama Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa mwenyewe alivyosema hivi karibuni: 'Afrika inabadilika kwa sababu fikra za umma na serikali zinabadilika.'
Kwa hakika, mchakato wa kuwafukuza wanajeshi wa Ufaransa, ulioanzia Mali na kufuatiwa na nchi kama vile Niger, Nigeria, Chad, Senegal, na Burkina Faso, sasa umefika Ivory Coast. Nchi hizi zimewafukuza rasmi wanajeshi wa Ufaransa katika nchi zao, zimefunga kambi zake za kijeshi na kutaka kutambuliwa kujitawala na matakwa ya mataifa ya Afrika kwa msingi wa kuheshimiana pande mbili. Taasisi ya Sera za Kimataifa ya Austria imeandika hivi kuhusiana na suala hilo: 'Hatua ya nchi za Kiafrika ya kuwafukuza wanajeshi wa Ufaransa ni sehemu ya mchakato mpana wa kutaka kujitawala na kusisitiza juu ya mamlaka zao za kitaifa.'
Janabo Sisse, mmoja wa watafiti wa Wakfu wa Utafiti wa Kimkakati, pia amesema katika muktadha huu kwamba: 'Uwepo wa kijeshi barani Afrika ulikuwa moja ya nembo za mwisho za nguvu ya Ufaransa, ambayo sasa imefifia.'
Katika zama hizi mpya, nchi za Kiafrika zinajaribu kutangaza rasmi mwisho wa zama za ukoloni wa Ulaya hususan Ufaransa barani humo kwa kupitisha sera za kupinga ukoloni na kuwa nchi huru na zenye nguvu katika mfumo wa kimataifa. Gazeti la Uswizi la "Luthan" limeandika hivi kuhusu suala hili: 'Katika miaka ya hivi karibuni, bara la Afrika limepitia mabadiliko ya haraka sana ya kijamii na kisiasa. Mchakato huu wa mwamko na ufahamu wa ghafla katika jamii ya Kiafrika umevuruga mitazamo ya jadi ya Ulaya kuhusu bara hili. Kufuatia mwamko huu, badala ya kukabidhiwa utajiri mkubwa wa nchi za Kiafrika kwa Wamagharibi, sasa vijana wanapigania demokrasia zaidi na mgawanyo wa kiadilifu wa rasilimali zao.