Ushiriki wa Nigeria katika BRICS ni muhimu, kwa nini?
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122482-ushiriki_wa_nigeria_katika_brics_ni_muhimu_kwa_nini
Uanachama wa Nigeria katika shirika la BRICS, kama "nchi mshirika" na yenye uchumi mkubwa zaidi katika bara la Afrika, ni suala muhimu na lenye taathira kwa bara hilo na mataifa yanayoinukia kiuchumi.
(last modified 2025-02-08T22:51:27+00:00 )
Feb 08, 2025 22:51 UTC
  • Ushiriki wa Nigeria katika BRICS ni muhimu, kwa nini?

Uanachama wa Nigeria katika shirika la BRICS, kama "nchi mshirika" na yenye uchumi mkubwa zaidi katika bara la Afrika, ni suala muhimu na lenye taathira kwa bara hilo na mataifa yanayoinukia kiuchumi.

Brazil, ambayo kwa sasa inashikilia uenyekiti wa zamu wa kundi la nchi za BRICS, imetangaza kuwa Nigeria imejiunga na kundi hilo kama "nchi mshirika." Mnamo Oktoba 2024, katika mkutano wa kilele wa BRICS uliofanyika huko Kazan, nchini Russia, iliamuliwa kuundwa kikundi cha nchi "washirika wa BRICS".

Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria, katika taarifa yake sambamba na kukubali rasmi mwaliko wa kujiunga na kundi la BRICS kama nchi mshirika, imetangaza kwamba: "Nigeria inakusudia kushirikiana na BRICS ili kuendeleza malengo ya pamoja katika nyanja za biashara na uwekezaji, usalama wa nishati, ustawi wa miundombinu, teknolojia na mabadiliko ya hali ya hewa."

Nigeria, iliyoko Afrika Magharibi, ni moja ya viituo muhimu vya kisiasa na kiuchumi vya bara hilo. Nigeria pamoja na Afrika Kusini, zinachangia zaidi ya humusi yaani moja ya tano ya wakazi wa Afrika, na zaidi ya asilimia 45 ya pato la kiuchumi la bara hilo.

Nigeria inatambuliwa kuwa uchumi unaoibukia au soko linaloibukia. Uchumi unaoibukia wa Nigeria una sekta zinazopanuka za viwanda, fedha, huduma, mawasiliano, teknolojia na elimu-burudani. Nigeria pia ina uchumi mkubwa na dhabiti katika bara la Afrika. Uwekezaji mkubwa wa China na Russia barani Afrika unawafanya wanachama wengine wa BRICS wawepo katika bara hilo, na hali hii imekaribishwa na kupongezwa na nchi nyingine za Afrika. Nigeria, yenye rasilimali na akiba kubwa ya madini, ni nchi inayofaa kwa uzalishaji wa bidhaa za kiteknolojia na pia utayarishaji wa malighafi za bidhaa za teknolojia ya juu, au teknolojia mpya na ya kisasa zaidi.

Ikiwa nchi mshirika wa BRICS, Nigeria inaweza kufanya jitihada za kupunguza utegemezi wake kwa sarafu ya dola ya Marekani na kuhimiza na kuimarisha biashara kwa sarafu yake yenyewe, jambo ambalo litasaidia kupunguza shinikizo la fedha za kigeni kwa serikali, ambalo ni moja ya matatizo ya uchumi wa Nigeria. Nigeria pia inaweza kuomba ufadhili wa miradi ya miundombinu kupitia benki ya BRICS, New Development Bank (NDB), kwa kuzingatia masharti maalumu.

Kama kambi ya chumi muhimu zinazostawi, BRICS inatoa fursa ya kipekee kwa Nigeria kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kijamii na kiuchumi na nchi wanachama. Nigeria ni nchi ya pili kujiunga na kundi la BRICS kama mshirika, baada ya Uganda. Uganda ilijiunga na BRICS kama mshirika mnamo Januari 1, 2025. Nchi mbili za Kiafrika yaani Misri na Ethiopia, pamoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu kutoka Ghuba ya Uajemi, pia zilijiunga na BRICS mwanzoni mwa 2024.

Iran ilikuwa mwanachama wa BRICS mwaka jana, 2024

Algeria pia inatarajiwa kutangaza jibu lake rasmi kuhusu kujiunga na BRICS kama nchi mshirika katika siku za usoni. Burkina Faso, Zimbabwe, Kongo, Morocco, Senegal, Chad, Equatorial Guinea na Sudan Kusini pia ni miongoni mwa nchi ambazo zimeonyesha nia ya kushiriki katika shughuli za BRICS na kuwa wanachama wa shirika hilo, na ziko katika safu ya kujiunga na BRICS.

Baada ya Afrika Kusini kujiunga na kundi la "BRIC" (Brazil, Russia, India na China) mwaka 2010 na kuligeuza kuwa "BRICS", uzito na nafasi ya bara la Afrika katika BRICS imeongezeka kutokana Misri na Ethiopia kuwa wanachama rasmi, huku Uganda na Nigeria zikiwa nchi washirika.

Nchi nyingine washirika wa BRICS ni Belarus, Bolivia, Cuba, Malaysia, Kazakhstan, Uzbekistan na Thailand. Mwaka huu, 2025, Indonesia imekuwa mwanachama kamili wa BRICS baada ya kuwa mshirika wa kundi hilo. Hamu ya nchi mbalimbali ya kutaka kujiunga na BRICS ni kielelezo cha kukua kwa nafasi na umuhimu wa shirika hili katika nyanja ya kimataifa. Nchi tofauti kutoka sehemu mbalimbali za dunia zinataka uanachama katika shirika hili, na BRICS imepata nafasi na umuhimu zaidi ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Uanachama wa nchi muhimu zenye uwezo maalumu wa kiuchumi, zikiwemo Iran, Russia, China, India na Afrika Kusini, pamoja na Brazil, katika BRICS, umepelekea nchi nyingine kutaka kuwa wanachama na kushirikiana na shirika hili ambalo sasa linajulikana kama nembo ya chumi huru na zinazoinukia haraka.